Mpango wa Annan na majaaliwa ya Syria
17 Aprili 2012Wachambuzi wanasema hivi sasa rais Assad anatumia nafasi ya kusitisha mapigano ambayo ni sehemu ya mpango huo wa hatua sita kuzidi kujiimarisha.
Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yanaonyesha ufanisi ingawa vikosi vya rais Assad vimeendelea kuushambulia mji wa Homs kwa makombora kwa siku kadhaa.
Ni mwanya ambao jumuiya ya kimataifa iko tayari kumuachia rais Assad kwa matumaini ya kumlaazimisha kuingia katika hatua nyingine ya utekelezaji wa mpango huo, ambayo ni mazungumzo na wapinzani wanaotaka kuondolewa kwake madarakani.
Assad asema katu hang'oki
Assad amesisitiza kuwa yeye haondoki na ametumia vikosi vya serikali kuwasambaratisha wapinzani na waasi wanaoendesha harakati za kupinga utawala wake kwa muda wa miezi 13 hadi sasa. Ingawa alikubaliana na mpango wa Annani, upo uwezekano wa yeye kutotekeleza mpango huo kutokana na kutokuwepo shinikizo la kutosha.
Hakuna tishio la kuvamiwa kijeshi na waasi hawana silaha za kisasa za kuweza kuutishia utawala wake. Assad anaungwa mkono na Urusi, China, Iran pamoja na makundi muhimu nchini mwake.
Hoja nyingine zinasema Mpango wa Annan umempa nafasi Assad kuzidi kujiimarisha. Shadi Hamid wa kituo cha Brookings mjini Doha, anasema hakuna dalili ya kuwepo matumaini huko mbele na kuongeza kuwa kama mwisho wa mchezo ni kuondolewa kwa Assad, hadhani kama mchezo huu uko karibu kabisaa na kumalizika.
"Mataifa ya Magharibi yanaunga mkono mpango huu ingawa yanajua kuwa utashindwa, kwa sababu pia hawako radhi kuazisha operesheni za kijeshi dhidi ya utawala wa Assad", anasema Peter Harling kutoka kundi la kimataifa la kutatua migogoro.
Kwa nini washirika wa Assad wanaunga mkono mpango huu?
Na wakati huohuo, washirika wa Assad wanaunga mkono mpango huu, kwa sababu tofauti na mpango wa Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Kiarabu mwanzoni mwa mwaka huu, mpango huu haumtaki Assad kukaa pembeni kupisha mazungumzo ya amani.
Tangu kuanza kwa utekelezaji wa hatua ya kusitisha mapigano wiki iliyopita, Syria imekiuka vipengele muhimu. Vifaru, wanajeshi na askari kanzu bado wanaendelea kuweka doria katika mitaa kwa lengo la kuwazuia wandamanaji licha ya Annani kudai majeshi kuondolewa mitaani na kurejeshwa kambini. Licha ya kupungua kwa machafuko, jeshi la Syria limeendelea kuushambulia mji wa Homs mwishoni mwa juma.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alisema siku ya Jumatatu kuwa atavumilia ukandamizaji wa Assad kwa sasa ili kuyapa nafasi makubaliano ya amani yaweze kuifikisha nchi hiyo kwa majadiliano ya kisiasa.
Umoja wa Mataifa umepanga kupeleka ujumbe wa waangalizi wapatao 250. Mpaka ni watu sita tu wamewasili nchini humo. Annan kwa maksudi, hajaweka bayana hadidu za rejea za mazungumzo kutokana na ukweli kuwa pande husika bado hazitambuani. Serikali ya rais Assad inawaita wapinzani kama majambazi na magaidi, wakati Baraza la kitaifa la Syria nalo linasema hakuna haja ya kuzungumza na Assad.
Viongozi wa upinzani wanasema wako tayari kuupa nafasi mpango wa Annani ingawa wanaamini Assad hana nia ya kuutekeleza. Kama Assad ataendelea kukiuka makubaliano, hii itaonyesha kuwa si mtu wa kuzungumza naye na kwamba dunia inahitaji kutumia nguvu dhidi yake. Na kama itatokea utawala huu ukaacha ukandamizaji, utapoteza udhibiti kwa kasi kutokana na jinsi wandamanaji watakavyofurika mitaani.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE
Mhariri: Mohammed Abdula Rahman.