Mpango wa Brexit wa Theresa May wapata pigo jingine
19 Machi 2019
Katika tangazo la kushtukiza jana jioni, Spika wa bunge la Uingereza John Bercow alisema wabunge hawawezi kuupigia kura mpango ule ule wa Brexit walioukataa awali katika msimu huu huu wa Bunge. Akitumia kigezo cha mwaka 1604, Spika huyo alisema itakuwa kinyume cha sheria kwa serikali kuwasilisha tena mpango uliokwishapingwa na wabunge.
Tangazo hilo la Spika Bercow limekuja wakati serikali ya Theresa May ikihangaika kuwashawishi wabunge kuukubali mpango huo wa Brexit ambao tayari wamekwishaubwaga mara mbili, ikitarajia kuwa ungepigiwa kura tena wiki hii.
Kuiwajibisha serikali
Bercow alitoa ufafanuzi kuhusu tangazo lake, akisema hataki lichukuliwe kama kauli ya mwisho kwenye mpango wa Brexit, bali kama sharti ambalo serikali inalazimika kulitimiza, ili yeye aweze kuandaa kura ya tatu bungeni kuamua juu ya mpango huo.
Waziri wa Brexit Steve Barclay akijibu tangazo la spika amesema hiyo inamaanisha kwamba yumkini hakutakuwa na upigaji kura wiki hii bungeni, na hiyo, ameongeza, inamaanisha kuwa Uingereza itachelewa kidogo kuondoka katika Umoja wa Ulaya.
''Ni uamuzi muhimu, ambao bila shaka unahitaji kutazamwa kwa makini. Tutautafakari kwa kina na tutachukua uamuzi ipasavyo.'' Amesema Barclay.
Chanzo kutoka katika serikali ya Bi Theresa May kimeliambia shirika la habari la AFP, kwamba hatua ya spika Bercow ni ishara kwamba anataka kuchelewesha Brexit kwa muda mrefu, ambapo bunge litachukua udhibiti wa mchakato mzima likinuia kufikia makubaliano laini na Umoja wa Ulaya.
Kiunzi kingine katika njia ya May kuelekea Brexit
Waziri Mkuu May alitazamia mpango wake ungeshinda kura ya tatu bungeni hapo kesho Jumatano, kabla ya kusafiri kwenda Brussels ambako ataomba kucheleweshwa kwa tarehe ya Uingereza kuondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya, hadi Juni 30 mwaka huu. Wabunge wengi wa chama cha Conservative ambao awali walipinga mpango wa Theresa May, walikuwa wameashiria kuukubali mara hii, kwa masharti mepesi.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hapo jana walikubaliana na dhana ya kuipa Uingereza muda zaidi, ila walitilia shaka nia ya ucheleweshaji huo.
Afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya amewaambia waandishi wa habari kuwa umoja huo unaweza kuridhia ombi la Uingereza kutaka muda zaidi wa mchakato wa Brexit, mradi ombi hilo liwasilishwe muda wowote kabla ya tarehe 29 Machi, na si baada ya saa tano usiku saa ya London.
Mwansheria mkuu wa Uingereza Robert Buckland amemkosoa vikali Spika wa bunge, akisema ameitumbukiza Uingereza katika mgogoro wa kikatiba.
afpe, rtre