1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kurudisha makwao wakimbizi wakosolewa Ujerumani

24 Machi 2017

Bunge la Ujerumani lavutana kuhusu muswada wa sheria juu ya kuwarudisha makwao wahamiaji walionyimwa hifadhi nchini,wabunge wengi wa upinzani waukataa muswaada huo

Berlin Vereidigung von Bundespräsident Frank-Walter Steinmeier
Picha: Reuters/H. Hanschke

Ujerumani inataka kuimarisha zaidi jinsi ya kulishughulikia suala la wahamiaji wanaoomba hifadhi lakini wakosoaji wa hatua hizo na wataalamu wanasema kwamba hatua ya kuwarudisha makwao wahamiaji mara nyingi huwa ni ya kikatili na yenye gharama kubwa.Suala hili limezusha mjadala mkubwa katika bunge la Ujerumani mjini Berlin hapo jana.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas De Maiziere alifika bungeni hapo jana na kutoa hoja zake mbele ya wabunge akiutetea muswaada mpya wa sheria ambao utaweka vigezo vikali kwa wanaoomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani.Waziri huyo alisema kwamba umma wa Ujerumani utaunga mkono tu sera za kuwapokea wahamiaji wanaotaka kuomba hifadhi nchini ikiwa serikali itaanzisha mpango sheria hiyo ya kuwarudisha makwao wale watakaokataliwa ukimbizi nchini  na kuilinda jamii ya Ujerumani dhidi ya uwezekano wa vitisho kutoka kwa wakimbizi.

De Maizeire amesisitiza kwamba muswaada huo wa sheria umechochewa na kisa cha mtuhumiwa wa ugaidi  Anis Amri raia wa Tunisia aliyehusishwa na mashambulizi ya soko la Krimasi Desema 19 mwaka jana katika eneo la Breitscheidplatz mjini Berlin tukio ambalo lilionesha umuhimu wa kutambuliwa na kurudishwa makwao pamoja na kufuatiliwa nyedo zao watu wanaotajwa kuwa  wenye uwezekano wa kuwa kitisho cha kweli kwa usalama nchini Ujerumani.

Akiendelea kuutetea muswaada huo De Maizeire amesema kwamba kuomba hifadhi na kurudishwa makwao watu waliokataliwa hifadhi ni mambo yanayokwenda sambamba huku pia alitetea mapendekezo ya kutumika data za  simu za wahamiaji hao.Kimsingi inapendekezwa kwamba ofisi za uhamiaji nchini ziwe na mamlaka ya kuzichunguza simu za waomba hifadhi ili kuwatambuwa hasa ni watu wa aina gani suala ambalo linafananishwa na  uchunguzi unaofanyiwa mtu katika idara ya forodha wakati mizigo inapokaguliwa mipakani.

Lakini De Maizeire amesisitiza kwamba kuchunguzwa simu za wahamiaji sio jambo lililopitiliza  bali ni suala linalofanyika kwa njia zinazozingatia haki.Wanaopinga muswaada huo wanasema kwamba ni sheria zinazonuiwa kutumika hasa kuongeza idadi ya wanaonyimwa hifadhi pamoja na kukiuka sheria za Ujerumani na hadhi  za wanaoomba hiofadhi.

Wakimbizi katika mradi wa elimu ya digitali kwa wahamiaji wa AfghanistanPicha: Getty Images/S. Gallup

Naibu spika wa bunge la Ujerumani Petra Pau wa chama cha Die Linke ameongeza kusema kwamba muswaada huo unaharibu kabisa mtazamo jumla uliopo katika kuunga mkono mpango wa kurudishwa makwao wakimbizi hao na kitendo hicho kinasababisha athari kwa wale wanaohitaji kulindwa huku akiweka wazi kwamba thuluthi moja ya wanaoomba hifadhi ni vijana walioo chini ya umri wa miaka 18.

Kwa upande mwingine wanaharakati wanaowatetea wakimbizi wanachukizwa na muswaada huo.Pau anasema kimsingi muswaada huo anaouita ''muswaada wa kijana Amri''haungeweza kuwa na dhima yoyote katika kuzuia tukio la ugaidi la Desemba mwaka jana mjini Berlin.

Mbunge wa chama cha Kijani Luise Amtberg pia akiupinga muswaada huo amesema umeandikwa vibaya na hausimamii haki kuelekea wakimbizi.Zaidi ya hilo ametetea msimamo wake akisema sheria hiyo inayopendekezwa na serikali ya Kansela Merkel imepuuza kuangalia ni kwa jinsi gani wageni walivyojumuishwa katika jamii licha ya kuweko mazingira magumu na juu ya hilo anasema ni mpango utakaochochea tu kuitenga idadi kubwa ya watoto kwenda shule.Muswaada huo unaopingwa na chama cha Die Linke na kijani unatarajiwa kupelekwa mbele ya kamati ya bunge kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho kabla ya kupigiwa kura ya mwisho na bunge.

MwandishiSaumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga

Source:DW English Page