1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Labour kufuta mpango wa wahamiaji wa Sunak kama itachaguliwa

10 Mei 2024

Kiongozi wa Chama Kikuu cha upinzani cha Labour nchini Uingereza Keir Starmer amesema hii leo wataufutilia mbali mpango wa serikali ya Conservative wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda ikiwa wataingia madarakani.

Keir Starmer I Kiongozi wa Labour
Kiongizi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour Keir Starmer ameahidi kufutilia mbali mpango wa serikali ya Rishi Sunak wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini RwandaPicha: Gareth Fuller/dpa/picture alliance

Chama hicho cha Labour kimeahidi badala yake kuanzisha mkakati mgumu zaidi wa kukabiliana na wahamiaji wasio na vibali ikiwa ni pamoja na kuanzisha kikosi kazi kipya cha mpakani na kuongeza nguvu ya kupambana na ugaidi. 

Kwenye hotuba yake aliyoitoa kwenye mji wa Dover, kwenye kaunti ya Kent, Kiongozi huyo wa Labour Keir Starmer aliitaja sera hiyo ya Waziri Mkuu Rishi Sunak kama hila tu na matumizi mabaya ya fedha na kuongeza kuwa mpango huo unataorajiwa kuanza Julai Mosi, hautaweza kulidhibiti tatizo.

Soma pia:Uingereza kuanza kuwapeleka wahamiaji Rwanda Julai Mosi 

"Tutaufuta huu mpango wa Rwanda. Niliwaambia hili tulipokutana mara ya mwisho wiki iliyopita. Na, unajua hiyo inamaanisha kuuondoa huo mpango, kabisa, ndege na kila kitu. Hautafanya kazi. Ni kuoteza tu pesa. Ni ulaghai, si suluhu," alisema Starmer.

Zaidi ya wahamiaji 8,800 wameingia Uingereza tangu Januari, 2024

Amesema, ni watu wachache tu walioondolewa, ambao ni chini ya asilimia moja ya wahamiaji wanaovuka bahari kwa kutumia boti ndogo kila mwaka na kuongeza kuwa pamoja na kujipambanua kisiasa, Sunak anataka tu kuwaridhisha wenye misimamo mikali ya kihafidhina wanaopinga uhamiaji. Lakini hata mbunge wa chama chake cha Conservative katika eneo hilo, Natalie Elphicke ameungana na Labour akisema sera hiyo haifanyi kazi.

Boti ndogo ikiwa imewabeba wahamiaji wanaopitia Ujia wa bahari unaotokea Ufaransa hadi Uingereza katika picha iliyopigwa Machi 6, 2024.Picha: Dan Kitwood/Getty Images

Zaidi ya watu 8,800 wameingia Uingereza kupitia Ujia wa bahari unaotokea kaskazini mwa Ufaransa hadi sasa, kuanzia mwezi Januari na kulingana na Starmer, karibu watu 30,000 wameingia nchini humo mwaka 2023 kwa kutumia boti ndogo.

soma pia: Bunge la Uingereza lapitisha sheria tata ya wahamiaji kupelekwa Rwanda

Starmer amesema ikiwa watachaguliwa, wataunda Amri mpya ya Usalama Mipakani, kwa kushirikiana na Shirika la Kitaifa la kushughulikia Uhalifu, Shirika la Uhamiaji, Idara ya Mashtaka ya Crown na MI5.

Ameongeza kuwa tayari ameanza kushinikiza kuwepo kwa mkataba mpya wa usalama na washirika wa Uingereza wa Ulaya, na akasisitiza haja ya ushirikiano mpya na polisi ya Ulaya, Europol, ambao serikali ya Uingereza ilijitenga nao kama sehemu ya makubaliano ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit.

Kiongozi huyo wa Labour amesema chini ya mpango wake mpya, mamlaka ya kukabiliana na ugaidi yataongezwa, yakijumuisha kuwasaka washukiwa wa biashara haramu ya binadamu kwa kuwawekea vikwazo vya kutembea pamoja na shughuli za kibenki kabla hata ya kufanya uhalifu huo.

Chama cha Labour, kinachopigiwa upatu kwa kiasi kikubwa kushinda uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu baada ya miaka 14 ya upinzani, kimekuwa kwenye shinikizo kubwa kikitakiwa kifafanue kile itakachokifanya ikiwa kitachaguliwa kushika dola.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW