1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Marekani kubadilishana wafungwa wakosolewa

2 Juni 2014

Makubaliano ya kuachiliwa huru mwanajeshi wa Marekani Bowe Bergdahl kwa kubadilishana na wafungwa wa Taliban kumezusha shutuma baada ya kiongozi wa wanamgambo hao kudai kuwa ni “ushindi mkubwa“,

Bowe Bergdahl Soldat Entführung Afghanistan
Picha: picture alliance/AP Photo

Mpango huo wa ubadilishanaji pia umeongeza matumaini ya kupatikana amani wakati Marekani ikijiandaa kuondoka kabisa Afghanistan. Marekani imetetetea mpango huo wa kubadilishana mwanajeshi wake na wafungwa watano wa Taliban, ikisema ulikuwa muhimu katika kuyaokoa maisha ya Sajenti Bowe Bergdahl, kwa sababu afya yake ilidhoofika kwa kasi baada ya miaka mitano ya kushikiliwa mateka na Taliban tangu vita vilipoanza mwaka wa 2001. Alikuwa mwanajeshi pekee wa Marekani aliyeshikiliwa mateka baada ya kuanza vita hivyo nchini Afghanistan.

Lakini mpango huo wa ubadilishanaji uliotangazwa Jumamosi umekosolewa na wabunge wa Republican, ambao wanasema wafungwa watano wa Taliban, ambao wote ni viongozi wa ngazi ya juu waliokuwa wakizuiliwa katika jela ya kijeshi ya Marekani ya Guantanamo Bay nchini Cuba, wanaweza kurudi tena katika uwanja wa mapambano na kuwa kitisho kwa Wamarekani wanaoishi ng'ambo.

Serikali ya Afghanistan imeshutumu kuachiliwa kwa Wataliban hao watano, ikisema kupelekwa kwao nchini Qatar kunakiuka sheria za kimataifa. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Afghanistan imesema serikali za Marekani na Qatar zilistahili kuwaachia wafungwa hao “bila masharti yoyote”.

Rais wa Marekani Barack Obama akiwa na wazazi wa mwanajeshi Bowe Bergdahl katika Ikulu ya White HousePicha: Reuters

Seneta John McCain, ambaye binafsi alikuwa mfungwa wa kivita nchini Vietnam, aliwataja wafungwa hao kuwa “magaidi sugu” akisema “inasikitisha kuwa wataweza tena kuwa kurejea katika uwanja wa vita”. Mullah Mohammad Omar, kiongozi wa kiroho wa Taliban, alitoa taarifa akisifu kuachiliwa kwa wafungwa hao wa Guantanamo akisema kuwa ni “ushindi mkubwa”, na akawapongeza wote.

Watalaamu wanasema mpango huo huenda ukapiga jeki juhudi za usalama, wakati Marekani ikijiandaa kuondoka nchni Afghanistan mwishoni mwa mwaka wa 2016, na kumaliza kabisa vita vilivyodumu muda mrefu zaidi wa miaka 15 baada ya mashambulizi ya Septemba 11.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ameelezea matumaini kuwa makubaliano hayo yanaweza kufungua njia ya kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Taliban, na kuziunga mkono juhudi zinazoongozwa na Afghanistan za kutafuta muafaka wa amani unaoweza kuwa muhimu katika kuzuia kuporomoka katika awamu ijayo isiyo na uhakika. Vikosi maalum vya wanajeshi vikisaidiwa na ndege za helikopta vilitumwa katika eneo lisilojulikana mashariki mwa Afghanistan ambako wanamgambo wa Taliban walimkabidhi Bergdahl.

Bergdahl aliwasili jana katika hospitali moja ya kijeshi ya Marekani mjini Landstuhl, kusini mwa Ujerumani ambako ataendelea kupewa matibabu. Maafisa wa Marekani awali walisema mwanajeshi huyo alikuwa katika hali “nzuri” na angeweza kutembea kivyake. Mazingira ambayo yalisababisha kutoweka mwanajeshi huyo kutoka kambi yao Mashariki mwa Afghanistan mwaka wa 2009 bado hayajulikani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW