Merkel Kommentar
2 Desemba 2011Hata baada ya hotuba yake Bungeni, ambayo ilikusudiwa kutoa ufafanuzi, bado Kansela Merkel amebakia kuwa haeleweki. Badala ya kuja na kutoa jibu la namna ya kuutatua mgogoro wa madeni katika Kanda ya Euro, ameendeleza mdahalo mrefu unaochosha wa kuufanyia mabadiliko Mkataba wa Umoja wa Ulaya. Hiyo, kwa hakika, siyo ishara iliyokuwa ikitarajiwa na masoko ya kifedha.
Vivyo ndivyo alivyokuwa mshirika wake, Rais Sarkozy, ambaye naye katika hotuba yake ya Toulon hapo jana, alibakia mtu asiye na uhakika wa akisemacho. Umoja wa kifedha uliotulia na wenye sheria kali ndiyo kauli inayowaunganisha viongozi wawili hawa, ambayo imewafanya wapewe jina la Merkozy na vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa viongozi, umoja huo wa kifedha wenye udhibiti wa hali ya juu kwenye bajeti za mataifa wanachama wa Kanda ya Euro yenye matatizo ya madeni, ni hatua inayopasa kuchukuliwa haraka. Lakini suala la marekebisho ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya kwa mnasaba wa kuepuka kitisho cha mpasuko ndani ya Umoja wa Sarafu, halina nafasi hapa.
Inaonekana kuwa serikali ya Ujerumani iko tayari kustahamilia kupanda kwa deni lake kupitia Benki Kuu ya Ulaya. Hadi sasa, benki hiyo inasalia kuwa taasisi pekee ya kifedha ambayo ni kiungo na dhamana cha mataifa yanayozama kwenye madeni.
Tangu mwanzoni mwa wiki, benki hiyo imekuwa ikinunua baadhi ya madeni ya mataifa hayo, lakini chini ya thamani. Inachota fedha kutoka mfuko wake mmoja, na kuziingiza katika mfuko wake mwengine, kwa kununua madeni ya Italia na Hispania. Mwisho wa hayo, ni mfumko wa bei, kupanda kwa gharama za maisha na kuporomoka kwa thamani ya sarafu.
Kansela wa Ujerumani na Rais wa Ufaransa hawana uhakika kama walivyokuwa mawaziri wao wa fedha mwanzoni mwa wiki. Mawaziri hao walifahamu kuwa, Mfuko wa Kuiokoa Kanda ya Euro, EFSF, na maneno machache ya kitaalamu, yanatosha kurudisha imani ya masoko.
Shirika la Fedha la Kimataifa lazima linajikuta kutumbukizwa kwenye suala hili, maana hadi sasa hakuna Shirika la Fedha la Ulaya. Huo Umoja wa Kifedha uliotulia, ambao unapiganiwa sasa na Merkel na Sarkozy, ni jambo lililotakiwa liwepo kwa mwaka mzima sasa. Laiti kama Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ingelipigania hilo hapo kabla!
Ama ikiwa mataifa mengine 27 yatakubaliana na mpango huu mpya wa Merkozy, bado ni suali lisilo jawabu. Lakini wakati huo huo, mgogoro unaoiandama sekta ya benki bado upo pale pale. Na hilo halijazungumziwa si na Merkel wala si Sarkozy. Kinachoonekana, badala yake, ni kwamba viongozi hao wawili wako tayari kuchukuwa uongozi wa kutupeleka wasikokujua.
Tangu kumalizika kwa mkutano wa kilele mwishoni mwa mwezi wa Oktoba, hakuna mengi yaliyoweza kufanywa. Deni la Ugiriki bado linabebwa na mabenki. Mpango wa kuweka ukomo wa kukopa kwa hazina za mataifa wanachama, bado upo kama ulivyokuwa hapo kabla. Uwezo kamili wa mfuko wa EFSF bado haujathibitika. Njia ya mataifa ya Ulaya kutoka kwenye ukuta wa madeni, bado haijaonekana. Na Merkel na Sarkozy wanaendelea kucheza na wakati.
Mwandishi: Bernd Riegert/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josphat Charo