Mpango wa rais Bush.
26 Septemba 2008WASHINGTON:
Mazungumzo juu ya mpango wa kutatua mgoro wa fedha wa Marekani yataendelea leo.
Hapo awali Seneta maarufu aliesema vyama vyote viwili vya kisiasa kwenye bunge la Marekani vinakubaliana kimsingi juu ya mpango wa rais G. Bush wa kutenga dola BILIONI 700 ili kuifufua sekta ya fedha inayokabiliwa na mgogoro mkubwa nchini Marekani.
Seneta huyo Christopher Dodd , ambae ni mwenyekiti wa kamati ya baraza la seneti inayoshughulikia masuala ya Benki ameeleza kuwa makubaliano ya kimsingi yamefikiwa juu ya mpango huo. Seneta Dodd anatumai bunge litapitisha sheria juu ya mpango huo mnamo siku chache zijazo.
Kabla ya hapo waziri wa fedha wa Marekani Henry Paulson alitoa mwito kwa wabunge wa vyama vya Demokratik na Republican kuwahimiza waondoe tofuati zao haraka ili makubaliano yafikiwe kwa lengo la kuyaokoa mabenki yaliyofilisika - hali inayotishia uchumi wa Marekani kusababisha vurumai kwenye mosoko ya fedha duniani kote.
Wakati huo huo waziri wa fedha wa Ujerumani bwana Peer Steinbrüch amesema Marekani inaweza kupoteza nafasi yake kama taifa kuu duniani, katika kuongoza mfumo wa fedha wa kimataifa kutokana na mgogoro huo wa fedha.
Akifafanua msimamo wa nchi yake juu ya mgogoro wa Marekani, waziri Steinbrüch kwa mara nyingine amesistiza mwito wake juu ya kuwepo udhibiti katika masoko ya fedha ya kimataifa.
Ameshuri haja ya kupiga marufuku uchuuzi wa hisa wa harakaharaka. Waziri huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa mgogoro wa Marekani umesababishwa na uroho wa kutaka kujipatia faida katika asilimia za tarakimu mbili pamoja na bonasi kubwa zinazotolewa kwa mameneja wa mabenki.