1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Trump umekubalika ila bado mgumu kuutekeleza

Amina Abubakar dpa/ap/afp/reuters
7 Oktoba 2025

Qatar imesema pande zote husika zinazojihusisha na juhudi za kusitisha vita Gaza zimeukubali mpango uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani, lakini imetahadharisha kuna baadhi ya changamoto ambazo hazijatatuliwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Qatar, Majed al-Ansari
Qatar yasema bado kuna mambo ya kutatua katika mpango uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu usitishaji vita GazaPicha: Imad Creidi/REUTERS

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Qatar, Majed al-Ansari amesema bado kuna vipengee katika mpango huo vinavyohitaji kufafanuliwa.

Akizungumza mjini Doha katika mkutano na waandishi habari, al-Ansari amesema kitu kigumu kufanya ni kuweka uhalisia wa mpango huo na kile kinachoendelea katika uwanja wa mapambano.

Majed al-Ansari ameongeza kuwa nchi yake imejikita katika jukumu lake la upatanishi na kuhakikisha kuwa mpango huo hatimae utafanikiwa kusitisha kikamilifu vita kati ya Israel na Hamas huku akisema Israel inapaswa kutarajia kuwa katika hili lazima kutakuwemo masharti ambayo hayakubaliki na pande zote.

Qatar imesema Israel inapaswa kutarajia kuwa katika usuluhishi lazima kutakuwemo masharti ambayo hayakubaliki na pande zote.Picha: Debbie Hill/Pool/REUTERS

"Kwa sasa tunashirikiana kwa karibu na Marekani kupitia wajumbe waliopo hapa Sharm el-Sheikh ili kufikia makubaliano ambayo yatahakikisha utekelezaji wa mpango huu hautakuwa wa muda mfupi, lakini -lengo sasa lazima luangazie namna ya kuugeuza mpango huu kuwa wa kivitendo na kufikia makubaliano madhubuti ambayo yanahakikisha hatua zinafanikishwa bila vikwazo vinavyoweza kutoa nafasi  kwa Israel kuanza tena vita vyake katika Ukanda wa Gaza."

Qatar yatambua juhudi za Marekani kusitisha vita Gaza

Msemaji huyo pia amezitambua juhudi za Marekani za kujaribu kusitisha mzozo wa Gaza. Amesema hatua ya mateka kurejeshwa Israel hilo pekee litaashirikia kukamilika kwa vita, kufuatia mpango wa Trump kufungamanisha hilo kama moja ya masharti ya kukamilika kwa mgogoro huo.

Masuala yanayoleta mvutano katika mpango huo yanahusisha kulipokonya silaha kundi la Hamas, na Israel kuwaondoa kikamilifu wanajeshi wake Gaza. Hamas imesema haitoweka silaha zake chini hadi pale Israel itakapowaondoa wanajeshi wake Gaza na kuitambua Palestina kama dola huru, jambo ambalo Israel imesema halitowezekana.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Qatar, Majed al-Ansari amezitambua juhudi za Marekani za kujaribu kusitisha mzozo wa Gaza.Picha: Muhammed Selim Korkutata/Anadolu/picture alliance

Qatar, Marekani, pamoja na Misri wameendelea kuongoza juhudi za upatanishi kati ya pande hizo mbili hasimu katika mgogoro huo, zikilenga kupata suluhu ya kudumu na kuzuwia mgogoro huo kutanuka zaidi katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.

Vita vya Israel na Hamas vyatimiza miaka miwili tangu vilipoanza

Haya yote yanajiri ikiwa ni miaka miwili tangu wanamgambo wa Hamas waliposhambulia Kusini mwa Israel na kusababisha mauaji ya waisraeli 1,200, huku wengine wakichukuliwa mateka, tukio ambalo ndilo lililochochea hali iliko sasa katika kanda hiyo.

Hivi leo (07.10.2025), raia nchini Israel walikusanyika pamoja kuwaenzi wote waliouwawa katika mkasa huo.

Raia wa Israel wakusanyika kuwaenzi wote waliouwawa katika mkasa shambulizi la Otoka 7 kusini mwa Israel lililotekelezwa na kundi la Hamas Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Lakini upande wa Gaza mambo yalikuwa tofauti, kwani wakaazi wa Ukanda huo wameadhimisha miaka hiyo kwa mashambulizi zaidi kutoka Israel.

Wakaazi wa Khan Younis iliyo kusini mwa Gaza na Gaza City iliyo upande wa kaskazini wamesema bado wameendelea kushambuliwa kutoka ardhini na angani.

Mwezi uliopita ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema inachokifanya Israel kwenye Ukanda wa Gaza ni "mauaji ya kimbari", huku makundi ya kutetea haki za binaadamu yakiishutumu pia Hamas, kwa kutekeleza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7. Pande zote mbili zinakanusha madai hayo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW