Mpasuko mkubwa muungano wa Tshisekedi, Kabila Congo
23 Oktoba 2020Katika kile kinachoashiria kuwa ni mvutano wa wazi baina ya rais Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila, Vuguvugu la FCC limetangaza leo kwamba liko tayari kusitisha muungano wake na chama cha UDPS cha rais Tshisekedi.
Kwenye taarifa ya vuguvugu hilo iliyosomwa na mbunge Didace Pembe, FCC imemtuhumu rais Tshisekedi kwa kukiuka maksudi katiba.
"Vuguvugu la FCC linaamini kwamba nia ya kukiuka katiba imetekelezwa kwa nia mbaya hadi mwisho na katika kutumia njia zote kwa nguvu. FCC iko tayari kubeba dhamana kutokana na wingi wa viti bungeni ilivyonavyo na kulingana na katiba,"
Kauli hiyo ya vuguvugu la FCC imetolewa saa kadhaa kabla ya rais Tshisekedi kuhutubia taifa baadaye Ijumaa.
Rais Tshisekediamefuta kikao cha baraza la mawaziri kilichopangwa kufanyika hii leo kama kawaida ya kila Ijumaa. Haijulikani ni uamuzi gani atakaouchukuwa rais Tshisekedi, lakini chama chake cha UDPS, tayari kimeomba kuvunjwa kwa bunge na baraza la mawaziri.
Soma pia: Maandamano Bukavu kumtaka Rais Tshisekedi kuheshimu katiba
Mbunge wa Kinshasa kutoka chama cha UDPS, Peter Kazadi ameiambia DW kwamba wamechoshwa na ushirikiano mgumu na chama cha FCC cha Joseph Kabila, ikikituhumu kutokuwa na nia nzuri.
Juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikiendeshwa kuwataka viongozi wa pande zote mbili kuyapa kipaumbele mazungumzo.
Tshisekedi akasirishwa na dharau za FCC
Duru kutoka ikulu ya rais Tshisekedi zinaeleza kwamba rais alikasirishwa na uamuzi wa waziri mkuu Sylvestre Ilunga na mawaziri wake kutohudhuria hafla ya kuapishwa kwa majaji watatu miongoni mwa tisa walioteuliwa na rais mwezi Julai.
Waziri mkuu na asilimia 65 ya mawaziri wa serikiali yake ni kutoka chama cha FCC cha Joseph Kabila. Wote walisusia hafla hiyo ya Jumatano. FCC ililaumu utaratibu wa uteuzi wa majaji hao ambao ilielezea kwamba ulikiuka katiba.
Soma pia: Vyama vya Tshisekedi, Kabila vyaanza kuvutana
Uhusiano baina ya rais Tshisekedi na maspika wa bunge na seneti ambao pia ni kutoka chama cha FCC, umekuwa wa panda shuka tangu rais Tshisekedi alipotangaza hali ya dharura nchini bila ridhaa ya bunge mwezi Machi kufuatia janga la Corona.
Katiba ya Kongo inaelezea kwamba rais anaweza kulivunja bunge baada ya mashauriano na waziri mkuu na maspika wa bunge na seneti. Mara litakapovunjwa, uchaguzi wa mapema wa bunge utatakiwa kuitishwa katika kipindi cha siku sitini.