1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Iran yatuhumiwa kuwashikilia wanaharakati kinyume cha sheria

Angela Mdungu
9 Oktoba 2023

Mpelelezi huru wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu Javaid Rehman, amesema Iran inawakandamiza waandamanaji na kuwashikilia wanaharakati wa haki za binadamu kinyume cha sheria.

Kiongozi wa juu zaidi nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei akiwa katika kikao kazi na maafisa
Kiongozi wa juu zaidi nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei akiwa katika kikao kazi na maafisaPicha: Iranian Supreme Leader's Office via ZUMA Press Wire/picture-alliance

Mpelelezi huyo mzaliwa wa Pakistan, amesema kati ya walioathiriwa na ukiukwaji huo wa haki ni pamoja na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobeli kwa mwaka 2023, Narges Mohammadi.

Rehman kupitia ripoti yake iliyosambazwa Ijumaa ameeleza kuwa Iran imekuwa pia ikitoa hukumu ya kunyongwa kwa idadi kubwa ya watu yenye kushtusha.

Ripoti hiyo  iliyoangazia hali ya mambo nchini Iran kuanzia Oktoba 2022, iliandikwa kabla ya kutangazwa kwa mshini wa tuzo ya Nobeli iliyokwenda kwa Narges Mohammadi ambaye ni mtetezi wa muda mrefu wa haki za wanawake.

Mohammadi kwa sasa yuko katika gereza maarufu la Evin katika mji mkuu, Tehran akitumikia kifungo cha miaka 16.

Soma zaidi: Iran inatajwa na jumuiya ya kimataifa kama nchi yenye rekodi mbaya ya haki za binaadamu na ukiukwaji wa haki za wanawake

Ripoti yakosoa mwenendo wa serikali

Katika ripoti yake, Rehman ambaye ni Profesa wa sheria za kimataifa  za haki za binadamu katika chuo kikuu cha Brunel cha jijini London amesema mshindi huyo wa tuzo ya Nobeli ni kati ya wanasheria na wapigania haki za binadamu waliofungwa jela kutokanana kazi zao.

Mpelelezi huru wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu Javaid RehmanPicha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Profesa huyo wa sheria amekosoa vikali matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyotumiwa na mamlaka za Iran katika kukabiliana na maandamano yaliyofanyika kote nchini humo mwaka 2022, baada ya kutokea kwa kifo cha Mahsa Amini, mwanamke mwenye miaka 22, aliyekamatwa kwa kosa la kukiuka kanuni za mavazi za Iran.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai, watu wasiopungua 537 wakiwemo watoto 68 na wanawake 48 walifariki dunia kwa maandamano, wengine mamia walijeruhiwa. Maelfu ya raia nchini humo wameripotiwa kukamatwa, au kufungwa.

Msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iran hakutoa jibu lolote alipoombwa kutoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo.

Rehman katika taarifa yake hiyo ameonesha kutokuridhishwa kwake na hatua ya Iran kutokufanya uchunguzi huru na wawazi kuhusu kifo cha Amini, au matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.

Amependekeza kuwa, kiongozi wa juu wa kidini wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, serikali, mahakama na bunge wakubali kuwajibika kwa kifo cha mwanamke huyo na hatua za haraka zichukuliwe.

Mpelelezi huyo huru aliyeteuliwa na  baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lenye makao yake mjini Geneva amependekeza pia kuwa, Khamenei na mamlaka za Iran zianzishe uchunguzi huru wa haraka kuhusu mauaji ya waandamanaji na kukomesha kila aina ya unyanyasaji ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia na uonevu wa waandamanaji wa kike.

Soma zaidi: Iran: Waandamanaji waadhimisha mwaka mmoja wa ukandamizaji wa vikosi vya usalama Zahedan

Kamata kamata inalenga kunyamazisha wakosoaji

Taarifa ya Rehman said, inabainisha kuwa, vikosi vya usalama viliwakamata takribani wanaharakati 576 wa haki za binadamu wakiwemo waalimu na mawakili kutoka vyama vya wafanyakazi na makundi ya walio wachache.

Mwanaharakati wa Iran Narges ashinda tuzo ya Nobel 2023

02:36

This browser does not support the video element.

Vitendo vya ukamataji na mashambulizi hayo vinaonekana kuwa vimekusudia kuwanyamazisha watetezi wa haki za binaadamu na wa haki za kiraia hasa kuhusiana na haki za wanawake wanaotaka uwajibikaji katika suala la kifo cha Mahsa Amini, imeeleza ripoti hiyo.

Kukamatwa na vitisho dhidi ya waandishi wa habari ni kati ya yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo iliyoonesha kuwa, hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai, waandishi 21 walikuwa gerezani wakiwemo Niloofar Hamedi na Elaheh Mohammad  ambao waliripoti juu ya kifo cha Amini.

Wanashitakiwa kwa kushirikiana na serikali ya Marekani yenye uadui na Iran na hivyo kuhatarisha usalama wa taifa pamoja na kujihusisha na propaganda dhidi ya mamlaka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW