Mpinzani wa Deby ataka matokeo ya uchaguzi Chad yafutwe
13 Mei 2024Masra ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa wiki iliyopita amewasilisha ombi kwenye Baraza la Katiba kutaka kura hiyo ibatilishwe. Succes Masra na chama chake Les Transformateurs wamesema matokeo ya uchaguzi yaliompa ushindi, rais Mahamat Iddriss Deby, ni udanganyifu mtupu.
Sitack Yombatina, makamu mwenyekiti wa chama hicho amesema kiongozi wao ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Chad anapewa vitisho na wafuasi wake wanakamatwa kiholela.
"Tangu matokeo yatangazwe, jiji la N'Djamena limezingirwa, limegubikwa na vurugu kila mahali. Mikoani wanachama wetu wameandamwa. Wanachama 76 wamekamatwana kuwekwa rumande. Unyanyasaji usiokuwa na jina unaendelea hapa nchini. Succès Masra ambaye bado ni Waziri Mkuu wa mpito lakini ametumiwa droni zinazomchunguza wakati wote. Kwa hadhi aliyonayo alitakiwa kupewa heshma angalau kwa sasa. Tumetulia na tumedhamiria. Tunachoomba ni ukweli wa matokeo ya uchaguzi." amesema Sitack.
Matokeo yaliotangazwa wiki iliopita na Tume ya Uchaguzi ya Chad yalimpa ushindi rais Mahamat Dedy kwa asilimia 61 ya kura, huku Masra akipata asilimia 18.5 ya kura hizo.