1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mradi mkubwa wa kusafisha fukwe za bahari waanzishwa India

21 Novemba 2017

Fukwe za bahari jijini Mumbai, nchini India zinatajwa kusheheni uchafu kupindukia zikigubikwa na takataka za kila aina. Wakati  watu wengi wakilalamika tu kuhusiana na tatizo hilo, mtu mmoja ameamua kuibadili hali hiyo.

Indien Beach clean-up, Mumbai
Picha: Chhavi Sachdev

Mtu huyo ameanzisha mradi mkubwa zaidi wa kusafisha fukwe za bahari duniani. 

India ina ukanda wa Pwani wa zaidi ya kilomita 7000, lakini cha kusikitisha, sio fukwe zote nchini humo zenye muonekana wa kuvutia. Na kwa hakika wakaazi wa mji wa Mumbai wamezifanya fukwe hizo sio zaidi ya majaa ya takataka.

Fukwe hizo zimejaa takataka - mifuko ya plastiki ya rangi mbali mbali , chupa na vifurushi vya chakula vimetapakaa kila mahali, mara nyingi huingizwa katika nyavu za zamani za uvuvi au vitambaa vya kuoza.

Watu wengi wameghadhabishwa na hali hiyo, wakiwa na hasira kwa serikali ya jiji kwa kutosafisha au kwa wale ambao wanatupa ovyo taka.

Kutokana na hali hiyo mwanamume mmoja ameamua kuacha kulalamika na badala yake, amechukua hatua mikononi mwake.

Kwa siku za kawaida Afroz Shah mwenye umri wa miaka 36, hufanya kazi kama mwanasheria wa katiba katika mahakama kuu ya Mumbai. Lakini inapofika wikendi, anasafisha fukwe. Yote haya yalianza miaka miwili iliyopita, alipohamia katika nyumba moja iliyokuwa ikielekea upande wa fukwe  ya bahari ya Versova mjini Mumbai. Alikuwa ameishi katika eneo hilo tangu utotoni akicheza kwenye fukwe hiyo, kwahivyo alifurahia kurudi huko.

"Mimi ni mpenzi wa bahari,” amesema. "kuwa karibu na maji kunanipa amani,na kunanipa furaha.”

Lakini muonekana wa fukwe hiyo anaouona kutokea dirishani kwake haukuwa ule alioutarajia. Aligundua kwamba kwenda matembezini kunatoa taswira mbaya ya eneo hilo kutokana na uchafu na takataka zilizorundikana.Anasema eneo hilo la bahari sio tu lina takataka za plastiki lakini pia limesheheni kinyesi  kwasababu uchafu wa kutoka mabomba ya maji taka hutupwa kwenye bahari hiyo.

Kuwa mabadiliko ya unachokitaka

Shah hakuogopa, akifuata falsafa ya Gandhi ya "kuwa mabadiliko ya unachokitaka,” alianzisha alichokiiita "Shram Daan” inayomaanisha kujitolea kufanya kazi kwajili ya taifa lako. Jirani yake mwenye umri wa miaka 84 alikubali kujiunga naye.

Makundi ya watu wajitolea kusafisha fuo ya bahariPicha: Chhavi Sachdev

Asubuhi moja, wawili hao walikwenda ufukweni na mifuko ya plastiki na glavu za mikononi  ili kukusanya takataka. Watu waliwatazama. "Baadhi ya watu walitucheka na wengine walituuliza kwanini tunafanya kazi ya serikali?” anakumbuka. Wengine wakapendekeza awasilishe malalamiko au kuishtaki serikali. Shah aliendelea tu.

Hiyo siku, walijaza mifuko miwili mikubwa ya takataka kwenye ufukwe huo. Polepole, watu zaidi wakaanza kujiunga nao.

Leo hii kiasi ya watu 300 wanajitolea na kuja kusafisha kila jumamosi na jumapili. Msaada wao umebadilisha kazi hiyo iliyoanzishwa na Shah kuwa mradi mkubwa zaidi wa usafi duniani. Kujitolea kwake katika kazi hii kumemfanya amebandikwa jina la bingwa wa umoja wa mataifa wa dunia.

"Zaidi ya asilimia 80 ya uchafu ndani ya maji unatoka ardhini,” amesema Doug Woodring, mwanzilishi wa muungano wa kufufua bahari. "ikiwa tunaendelea kuijaza bahari na taka, itaendelea kuturudishia kwa mawimbi na upepo.”

Duniani, tani milioni nane za plastiki huingia baharini kila mwaka, hasa kwa njia ya vifaa vya ufungaji, chupa, sigara.

"Uzalishaji wa plastiki duniani umeongezeka mara mbili zaidi ya miaka kumi na tano iliyopita, ikifikia zaidi ya tani milioni mia tatu kwa mwaka,” amesema Gerhard J. Herndi, profesa na mwenyekiti wa biolojia ya majini katika chuo kikuu cha Vienna.

Wakati takataka nyingi za fukwe jijini Mumbai hutoka baharini, nyingi hutoka kwa wenyeji. Hivyo lengo la pili la Shah ni kuongeza ufahamu kuhusu matumizi ya plastiki kwa kuihusisha jamii.

"Kusafisha fukwe kutokana na taka za plastiki kwa hakika ni njia ya kwanza ya kufanya fukwe ivutie tena, lakini muhimu zaidi inatoa uelewa wa kutotupa plastiki katika mazingira, anasema Herndl.

Katika ufuo wa bahari wa Versova, wadogo kwa wakubwa, tajiri kwa masikini sasa wameungana bega kwa bega kufanya usafi na kuokota plastiki, wenyewe wakiona athari za kutupa plastiki.

Shah na wenzake walojitolea tayari wamekusanya zaidi ya tani 7,000 za takataka na serikali ya jiji sasa inatuma vifaa vya kuchimba na matrekta kusaidia kusafirisha plastiki kwenye eneo la ugawishaji wa taka, ambapo chochote kinachoweza kutumika kinatolewa.

Kando na kazi yake, Shah huandaa warsha katika vyuo na shule, mashirika yasiokuwa ya kiserikali zinamkaribisha kuzungumza juu ya athari za plastiki na utupaji taka.

Mwandishi: Fathiya/Sachdev Chhavi/DW

Mhariri:Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW