1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mradi wa kupambana na jangwa kuwapatia wakaazi wa Misr maeneo ya kilimo.

Sekione Kitojo31 Julai 2007

Unaweza kupanda chochote hapa, anasema Mohammed Ahmed mwenye umri wa miaka 76, akinyoosha mikono yake kuonyesha eneo lililomea mimea pamoja na miembe ambayo imesheheni maembe karibu kuvunja matawi. Lakini anaendelea kusema Mohammed alipofika mwanzo katika eneo hilo halikuwa na kitu bali jangwa tupu.

Eneo hili lenye mandhari yakupendeza liko katika barabara inayounganisha mji mkuu wa Misr Cairo na mji ulioko katika pwani wa Alexandria.

Ahmed alihama kutoka katika eneo lake la asili la kabila la Bedouin katika rasi ya Sinai na kuhamia katika eneo hilo kwa ahadi ya kupatiwa kazi pamoja na tangazo la wakati huo rais wa Misr Anuar Saadat kuwa ataiongoza nchi hiyo kulishinda jangwa. Alipata kazi katika kituo cha maendeleo katika jangwa, kituo cha utafiti kinachoendeshwa na chuo kikuu cha Marekani mjini Cairo.

Miaka 30 baadaye , Misr bado inapambana na jangwa, ili kutoa kazi na mahali pa kuishi kwa wakaazi wake ambao idadi yao inazidi kuongezeka.

Hata hivyo baadhi ya wanauchumi na walinzi wa mazingira wanahofu kuwa juhudi za nchi hiyo za kulifanya jangwa kuwa mahali panapomea majani ni ushauri usiofaa.

Shirika la umoja wa mataifa la chakula na kilimo linakadiria kuwa kiasi cha asilimia 96 ya nchi ya Misr liko katika jangwa la Sahara , na sehemu iliyobaki , ambayo ina rutuba iko katika eneo la mto Nile ambao unapatikana katika eneo la mashariki ya nchi hiyo. Pamoja na kwamba bonde la mto Nile linafanya kiasi cha asilimia nne tu ya eneo la nchi ya Misr , lakini eneo hilo linaishi karibu watu wote wa nchi hii wapatao milioni 79 na msongamano huo katika bonde hilo unaonekana kufikia katika hali mbaya , ikitiliwa maanani kuwa idadi ya watu nchini Misr itaongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050.

Hii imesababisha maafisa nchini humo kuanzisha mpango wa kuwahamishia watu katika eneo kubwa zaidi katika mradi wa Toshka. Matumaini ni kuwa katika muongo mmoja ujao, kiasi cha watu milioni sita watahama kutoka katika bonde la mto Nile na kupelekwa katika maeneo yanayomea mimea jangwani, kusini magharibi ya nchi hiyo na kupata kazi katika utengenezaji wa vifaa vidogo vidogo. Ukosefu wa kazi unafikia asilimia 9.3 nchini humo.

Ardhi itamwagiliwa maji , kwa maji yatakayoletwa kwa mabomba kutoka mto Nile kiasi cha kilometa 300 , pamoja na maeneo mengine ya karibu. Chini ya mpango huo utakaogharimu kiasi cha dola bilioni 70, maafisa wanapanga kutayarisha hekta milioni 1.4 kati ya hekta 95.5 milioni nchini humo katika miaka kumi ijayo.

Mradi huu wa Toshka umeweza kupata kujengwa kwa kituo kikubwa kabisa dunia cha kusukuma maji katika eneo la magharibi la jangwa, ikiwa ni sehemu ya maendeleo ya jangwa la Sahara, mradi uliozinduliwa mwaka jana na rais Hosni Mubarak. Kituo hicho cha kusambaza maji ambacho kiko kilometa 1,300 kusini magharibi ya mji wa Cairo , kina uwezo wa kusukuma mita za ujazo 14.5 milioni za maji kila siku kutoka ziwa Nasser, lililoko karibu na bwawa la Aswan, karibu na mpaka wa Misr na Sudan.

Misr inahitaji kulitumia jangwa ili kuwapa makaazi wakaazi wake ambao wanaongezeka kwa kasi. Pia tunapaswa kulitumia jangwa ili kuzalisha mazao ya chakula , ambacho tunaagiza kutoka nje, amesema Adly Bishai, muasisi wa kituo hicho cha maendeleo ya jangwa. Hali hii inapata nguvu zaidi kutokana na ukweli kuwa serikali haihitaji raia wake kulipia gharama za maji. Chini ya mfumo wa sasa, wakulima hawalipi gharama za upelekaji, matumizi ama mifereji ya umwagiliaji maji na hakuna mita za maji katika majumba mjini Cairo. Badala yake malipo ya maji yako katika msingi wa idadi ya vyumba katika nyumba.

Viwanja vya mchezo wa golf, pamoja na ukoka uliotunzwa vizuri, na kuzuwia jamii katika miji ya Misr, ni mifano ya namna inayotia shaka ya udhibiti wa maji katika nchi hii iliyoko jangwani.

Mlinzi wa mazingira ya jangwa Mostafa Saleh anaamini kuwa maafisa wanapaswa kuangalia zaidi utalii wa kimazingira katika juhudi zao za kuhakikisha hali nzuri ya baadaye nchini humo. Anasema kuwa thamani ya chemchem ya maji Oasis, kama kivutio cha utalii inaweza kuleta fedha nyingi zaidi kuliko ekari 400 za mashamba ya mpunga, na pia ni rahisi kulinda mazingira na kuendelezwa.