Mradi wa maji wa Umoja wa Ulaya kuwekwa wazi
9 Machi 2008Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imeashiria kuwa itachukua hatua kuyashughulikia madai kwamba kampuni binafasi zimependelewa katika mpango wa misaada wa kuboresha huduma za maji barani Afrika. Kiasi euro milioni 500 zimetolewa kwa ajili ya miradi katika nchi za Afrika, Karibik na Pacific. ACP, chini ya mradi wa Umoja wa Ulaya wa kuboresha huduma za maji uliopendekwa mnamo mwaka wa 2003 na aliyekuwa rais wa halmashauri ya umoja huo wakati huo, Romano Prodi.
Jinsi fedha hizi zilivyotumika imetiliwa shaka katika ripoti ya uchunguzi uliofanywa mnamo mwaka wa 2005 baada ya ombi la halmashauri ya umoja wa Ulaya na iliyochapishwa miaka miwili baadaye.
Moja kati ya malengo makubwa ya mradi huo wa maji lilikuwa kuboresha uwezo wa watu maskini kuyafikia maji safi kwa kuongeza udhamini wa sekta binafsi kuhusika katika ugavi wa maji. Lakini uchunguzi huo wa mwaka 2005 unasema kampuni zinasita kufanya miradi katika nchi za Afrika, Karibik na Pacific kwa sababu ya wasiwasi ikiwa zinaweza kupata faidi zinapowekeza.
Juma lililopita maafisa wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya walithibitisha wako tayari kurekebisha hali hiyo kwa kutoa fedha zaidi kwa miradi ya maji inayoongozwa na kampuni za umma. Miradi inayohusisha ushirikiano kati ya kampuni za umma barani Ulaya na za mataifa ya Afrika, Karibik na Pacifik, zinaweza kupewa kipaumbele. Pendekezo moja linalofikiriwa ni kwamba wakati fedha zitakapoongezwa, hadi asilimia 10 ya fedha hizo zitatengwa kwa ajili ya miradi ya sekta ya umma.
Wanaharakati wa kupambana na umaskini wamelalamika hakuna ushirikiano kati ya kampuni za umma za maji ambao umekuwa ukidhaminiwa na mradi huo wa Umoja wa Ulaya kufikia sasa. Wanaharakati hao wanasumbuliwa na upendeleo wa umoja huo kwa kampuni za kibinafsi, ikizingatiwa kwa sehemu kubwa kampuni hizo zimeyafanya maji kuwa ya gharama kubwa ambayo watu maskini hawawezi kuimudu.
Kwa mfano wakati kampuni ya Suez ya Ufaransa ilipopewa jukumu la ugavi wa maji katika miji nchini Afrika Kusini wakati wa miaka 1990, gharama iliyotozwa kwa huduma za maji ilipanda kwa asilimia 600.
Olivier Hoedeman, msemaji wa shirika la Corporate Europe Observatory, linalochunguza ushawishi wa biashara kwa wanaounda sera za Umoja wa Ulaya, amesema shirika hilo limeikaribisha hatua ya halmshauri ya umoja huo. Inaonekana halmashauri hiyo iko tayari kwa mabadiliko akihoji ingekuwa vyema ikiwa mfuko tofauti ungeundwa kudhamini ubia kati ya kampuni za kibinafsi.
Sera ya maji ya Ulaya yajadiliwa
Sera ya maji ya Umoja wa Ulaya ilijadiliwa kwenye mkutano uliofanywa katika bunge la Ulaya mnamo tarehe 6 na 7 mwezi Machi mwaka huu njini Brussels Ubelgiji. Marc Laimé, mwandishi wa habari anayejishughulisha na maswala ya maji aliuambia mkutano huo kwamba matatizo ya kuyafikia maji mara kwa mara yanakuwa magumu hata barani Ulaya. Watu takriban milioni 140 au asilimia 16 ya idadi ya wakaazi barani Ulaya hawana maji safi kwa ajili ya matumizi.
Hali hii huenda ikazidi kuwa mbaya kwa sababu ya mabadiliko ya hali hewa. Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, ukame umeugharimu uchumi wa Ulaya kati ya euro bilioni 85 na bilioni 100. Ukame ulioliathiri bara la Ulaya mwaka wa 2003 ulikuwa miongoni mwa ukame mbaya, na uliwaathiri watu karibu milioni 100 na kusababisha hasara ya kiuchumi ya euro bilioni tisa.
Christine Franck, mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayomilikiwa na umma ya Vivaqua nchini Ubelgiji anasema nchi yake inatoa mfano mzuri wa ugavi wa maji. Makaazi mjini Brussels hulipa bei iliyo chini kwa asilimia 25 kwa ajili ya maji ikilinganishwa na bei ya mjini Paris Ufaransa, huku kampuni hiyo ikilenga kuuza maji kwa bei nafuu zaidi hata kwa watu wasiojiweza.
Idadi wa wafanyakazi wa kampuni hiyo imeongezeka kwa asilimia 17 katika miaka mitano kwa sababu imepanua shughuli mpya kama vile ukarabati wa mifereji ya maji inayovuja.
Mwanasiasa wa mrengo wa kushoto katika bunge la Ulaya raia wa Italia, Roberto Musacchio, amesema serikali nyingi zinasita kutambua kwamba ipo haja ya kuwepo na haki msingi ya kuyafikia maji safi. Tunahitaji kulizindua wazo kwamba maji sharti yatangazwe kuwa haki ya binadamu. Barani Ulaya maji bado ni ya umma jambo ambalo Musacchio amesema lazima liendelezwe. Kwa hiyo kutoyatangaza maji kuwa haki ya binadamu kunapingana na msimamo huo.