1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mrengo wa shoto wadhibiti baraza la Seneti Ufaransa

26 Septemba 2011

Vyama vya mrengo wa shoto vimefanikiwa kulidhibiti baraza la Seneti kutoka vyama vya mrengo wa kulia nchini Ufaransa kwa mara ya kwanza katika historia katika uchaguzi uliofanyika jana.

Baraza la seneti la Ufaransa lenye wajumbe 348 linavyokaa katika kikao chakePicha: AP

Vyama vya mrengo wa shoto nchini Ufaransa vimefanikiwa kulidhibiti baraza la Seneti kutoka vyama vya mrengo wa kulia katika uchaguzi uliofanyika jana. Vyama hivyo vimepata wingi wa kutosha katika baraza hilo la Seneti kwa mara ya kwanza kwa muda wa zaidi ya miaka 50, ikiwa ni pigo kwa rais wa sasa mhafidhina Nicolas Sarkozy.

Miezi saba kabla ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa, chama tawala cha rais Nicolas Sarkozy kimepuuzia kile ilichosema kuwa ni ushindi mdogo, wa zaidi ya viti vitatu katika baraza hilo, kwa mujibu wa maafisa kadha kutoka chama cha rais Sarkozy.

Pigo kubwa kwa Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy miezi saba kabla ya uchaguziPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa masuala ya uhusiano katika bunge , Patrick Ollier, amesema kuwa matokeo hayo hayana umuhimu wowote wa kisiasa kitaifa. Kutokana na matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo wa baraza la seneti yaliyotangazwa leo Jumatatu, chama cha kisoshalist na washirika wake wa Kikomunist na walinzi wa mazingira, Greens wameshinda viti vya kutosha kuupa upande huo wa vyama vya mrengo wa shoto udhibiti wa baraza hilo kwa mara ya kwanza katika historia ya ufaransa.

Viti vyao katika baraza la seneti vinavyofikia jumla ya 177 ni wingi wa viti viwili zaidi ya vile 175 vinavyohitajika kuwa na wingi wa kutosha. Wasoshalist wanamatumaini kuwa hiyo itakuwa ni hatua kuelekea ushindi wa uchaguzi wa rais utakaofanyika katika muda wa miezi saba ijayo.

Nicolas Sarkozy ataingia katika historia akiwa kama rais ambaye ameupotezea mrengo wa kulia wingi wao katika baraza la seneti, amesema hivyo Francois Hollande, ambaye anafikiriwa kuwa huenda akashinda katika uteuzi wa mgombea wa chama cha kisoshalist ambaye atapambana na Sarkozy katika uchaguzi mkuu mwakani.

Francois Hollande, anayefikiriwa kuwa huenda akateuliwa na chama cha kisoshalist kugombea kiti cha urais mwakaniPicha: AP

Vyama vinavyotawala vya mrengo wa kulia vimekubali kushindwa mara baada ya kuwa wazi jana Jumapili kuwa mrengo wa shoto umefikia wingi wa viti 175.

Baraza la seneti halichaguliwi na wapiga kura wote, bali na wapiga kura maalum ambao ni maafisa waliochaguliwa kutoka idadi ya mameya 72,000, pamoja na madiwani wa mitaa na miji , wakiwapigia kura wagombea kwa msingi wa orodha ya majimbo.

Waziri mkuu Francois Fillon amekiri kuwa mrengo wa kulia umepata pigo kutokana na mgawanyiko uliopo na kwamba upande wa mrengo wa shoto umepata mafanikio makubwa.

Fillon amesema katika taarifa kuwa ukweli utajulikana mapema mwakani. Mpambano umeaza sasa.

Vyama vya mrengo wa kulia vimedhibiti baraza la seneti tangu mwaka 1958, ilipoundwa jamhuri ya tano nchini Ufaransa. Kabla ya uchaguzi , spika wa baraza hilo Gerard Larcher alikuwa na imani kuwa chama tawala kitabakia na kiasi ya viti sita hadi 12 ili aweze kuchaguliwa tena katika wadhifa huo hapo Oktoba mosi wakati baraza hilo litakapokutana. Lakini amekiri kuwa iwapo ameshindwa na upande wa mrengo wa shoto itakuwa ni kama tetemeko la ardhi kisiasa na matayarisho kwa ajili ya uchaguzi wa rais yatabadilika.

Mwandishi : Sekione Kitojo /afp

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman