1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko na moshi Fukushima

14 Machi 2011

Mripuko mpya umesikika katika kinu cha nyuklia cha Fukushima Daiichi asubuhi ya leo na kusababisha moshi kutanda hewani.

Kinu cha Nyuklia cha FukushimaPicha: AP

Shirika la usalama la nyuklia nchini humo limesema haliwezi kudhibitisha iwapo mripuko huo wa kemikali ya hydrogen katika kinu nambari 3, kilitokana na uvujaji ambao haukudhibitiwa wa miale ya nyuklia. Haijulikani pia iwapo mripuko huo umeathiri kinu hicho.

Picha: dapd

Idadi ya watu waliofariki kwenye tetemeko la ardhi na tsunami lililotokea siku ya Ijumaa kaskazini mwa Japan, imeongezeka na kuwa watu zaidi ya 3,200.

Shirika la kitaifa la polisi nchini Japan linasema kuwa idadi ya watu waliofariki kwenye tetemeko hilo inatarajiwa kuongezeka huku maelfu zaidi wakiripotiwa kupotea mashariki mwa pwani.

Picha: dapd

Usalama wa vinu

Kando na idadi hiyo ya watu waliofariki, maafisa wa serikali pia wanang'ang'ana kujaribu kudhibiti uwezekano wa kuyeyuka mafuta kwenye vinu vitatu tofauti vya nyuklia. Katika kinu cha kwanza cha Fukushima, majenereta matatu ya kukipowesha kinu hicho hayafanyi kazi. Kampuni inayovihudumia vinu hivyo, Tokyo Electric Power, inatumia maji ya baharini kuvipowesha vinu viwili na inajitayarisha kufanya hivyo kwenye kinu cha tatu.

Waziri mkuu nchini humo Naoto Kan amelitaja janga hilo kuwa baya zaidi nchi hiyo imewahi kushuhudia tangu vita vya dunia vya pili.

Waziri mkuu wa japan Naoto KanPicha: AP

Alisema kuwa huu ni wakati mgumu kwa taifa hilo katika miaka 65 lakini anaamini kuwa taifa hilo litafanikiwa kukabiliana na janaga hilo iwapo patakuwa na ushirikiano.


Mamia kwa maelfu ya watu wanakabiliwa na ukosefu wa chakula, maji na matatizo ya nguvu za umeme, huku kukiwa na baridi kali. Masoko ya fedha yanatarajiwa kufunguliwa kama kawaida hii leo, na benki ya Japan ipo tayari kutumia mitaji katika uwekezaji ili kuyaimarisha.

Mripuko wa volcano

Wakati huo huo mlima wa Volcano kwenye kisiwa cha Kyushu kilomita 1,500 kutoka eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi siku ya Ijumaa, unatoa moshi na mawe kwa mara nyengine tena. Shirika la utabiri wa hali ya anga limetoa onyo hapo jana kuwa mlima huo wa Shinmoedake umeanza kuchemka baada ya kutulia kwa wiki kadhaa.Haikubainika wazi iwapo mripuko huo wa Volcano unatokana na tetemeko hilo la ardhi.

Mwandishi: Maryam Abdalla/dpae/ ard/ ape

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW