Mripuko wa bomu wauwa wanne Pakistan
10 Aprili 2023Takriban watu wanne wameuawa leo hii na wengine 15 kujeruhiwa baada ya kutokea mripuko wa bomu katika jimbo la kusini magharibi la Balochistan nchini Pakistan.
Bomu hilo lililenga gari ya polisi katika soko lenye shughuli nyingi huko Quetta, mji mkuu wa Balochistan, ambao ni maskani ya waasi kadhaa wanaotaka kujitenga na wenye itikadi kali.
Afisa wa polisi, Azfar Mehsar, amesema uchunguzi wa awali unaonesha mripuko umesababishwa na bomu lililotegwa kwenye pikipiki na kufyatuliwa kwa rimoti. Hakuna kundi lililokiri kuhusika na mauwaji hayo.
Kwa miaka mingi, Pakistan imekuwa ikipambana na uasi wa wanamgambo wa Balochistan ambao wanadai sehemu ya utajiri wa jimbo hilo, pamoja na mashambulizi ya kundi la Tehreek-e-Taliban Pakistan, Wataliban wa Pakistan.