Mripuko wa Volcano wazua taharuki mjini Goma
23 Mei 2021Shirika la Habari la Taifa nchini Rwanda limeripoti kuwa karibu watu 3,000 kutoka mji wa Goma tayari wamevuka mpaka na kuingia kwenye wilaya ya Rubavu nchini Rwanda.
Shirika hilo limenukuu mamlaka za uhamiaji kwenye mpaka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Duru kutoka wilaya ya Rubavu zinasema waliowasili wamehifadhiwa kwenye majengo ya shule na maeneo ya ibada ambayo yalianza kutayarishwa tangu taarifa za kutokea mripuko wa Volcano zilipofahamika.
Balozi wa Rwanda nchini Congo Vincent Karega ameandika kwenye ukurasa wa Twitter kuwa "mipaka iko wazi na majirani hao wanakaribishwa kwa amani"
Mji wa Goma wanusurika na tope la Volcano
Wakati hayo yakijiri mjini Goma kwenyewe taarifa zinasema tope la moto ambalo limekuwa likititirika tangu kuripuka kwa Volcano ya mlima Nyiragongo limeishia nje kidogo ya mji Goma.
Hayo ni kulingana na Gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini Jenerali Constant Ndima.
Kiongozi huyo amesema tope hilo limekifikia kitongoji cha Buhene na mji wa Goma umenusurika. Ndima pia amearifu tathmini ya awali inaonesha watu watano wamefariki dunia hadi sasa.
Shirika la Habari la AFP limeripoti kuwa watu wameanza kurejea kwenye makaazi yao mchana huu baada hali ya taharuki na wasiwasi kupungua kwa sehemu fulani.
Mkaazi mmoja aliyehojiwa na AFP amesema ingawa watu wanarejea polepole, walio wengi bado wana hofu na mamlaka za eneo hilo hazijatoa taarifa yoyote rasmi tangu kulipokucha.
Mkaazi mwingine amesema bado kuna harufu ya kemikali ya Sulphur inayotokana na tope la volcano na mlima Nyiragongo umesalia kuwa na rangi nyekundu inayoashiria Volcano bado inaripuka.
Rais Tshisekedi anarejea nyumbani kuratibu msaada wa dharura
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Congo umesema umerusha ndege juu ya mji wa Goma kutathimini hali ilivyo lakini hadi sasa tope la Volcano halijaufikia mji huo lakini tahadhari kubwa inachukuliwa.
Rais wa Congo Felix Tshisekedi amesema anakatisha ziara yake barani Ulaya na anarejea nyumbani kuratibu juhudi za kutoa msaada wa dharura.
Wakati mkasa huo ulipotokea usiku wa kuamkia leo kulikuwa na hali ya taharuki na maelfu ya watu walionekana wakikimbia kunusuru maisha yao.
Baadhi yao walijihifadhi kwenye boti zilizo ndani ya ziwa Kivu na wengine walikimbia na kupanda mlima Goma ambalo ni uwanda wa juu kabisa katikati ya mji wa Goma.