Mripuko wajeruhi 80 mkutano wa waziri mkuu wa Ethiopia
23 Juni 2018Mripuko huo ulisikika muda mchache baada ya Abiy kumaliza hotuba yake katikati ya Addis Ababa, na kuwasababishia watu kukimbia kunusuru maisha yao. Waziri mkuu huyo aliwahiwa kukimbizwa akiwa salama.
Awali Abiy alikuwa ameliambia shirika la habari la FBC kuwa "watu wachache wameuawa na ni mashahidi wa upendo na amani," lakini taarifa za baadaye kutoka ofisi yake zilisema hakuna aliyepoteza maisha kwenye mripuko huo.
Waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 42 alisema mripuko huo "yalikuwa mashambulizi yaliyopangwa vyema lakini yaliyoshindwa." Hata hivyo, hakurusha lawama zake kwa kundi lolote, ingawa alisema polisi wanaendelea na uchunguzi, akiongeza kuwa "mashambulizi hayo yalikuwa ya kitoto na yasiyokubalika. Daima mapenzi yatashinda. Kuwauwa wengine ni kushindwa. Kwa wale wanaojaribu kutugawa, nataka kuwaambia kuwa hamujafanikiwa."
Mripuko huo kwenye Uwanja wa Meskel uliokuwa umejaa watu mjini Addis Ababa, ulitokea baada ya wiki kadhaa za mageuzi makubwa kabisa ambayo yamewashitua wengi kwenye taifa hilo la pili kwa idadi ya watu barani Afrika, na baada ya miaka kadhaa ya hasira kali dhidi ya serikali, hali ya hatari, watu kukamatwa ovyo na kufungiwa kwa huduma za intaneti.
Waziri mkuu ndiye aliyelengwa?
Mara tu ulipotokea, watu walianza kuwashambulia polisi waliokuwepo kwenye mkutano huo, huku wakipiga mayowe: "Woyane chini, chini, Woyane ni wezi", wakitumia jina la dhihaka dhidi ya serikali, na kuwashutumu polisi kujaribu kuirejesha nchi kwenye machafuko.
Sababu ya mripuko huo hadi sasa haijaelezwa, lakini mmoja wa waandaaji wa mkutano huo wa hadhara aliliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba yalikuwa mashambulizi yaliyomlenga waziri mkuu binafsi.
"Waziri mkuu ndiye aliyekuwa shabaha ya tukio hili," alisema Seyoum Teshome, akiongeza kwamba: "Kuna mtu alijaribu kurusha bomu la mkono kwenye jukwaa ambako waziri mkuu alikuwa amekaa, lakini akazuiwa na umati wa watu." Kwa mujibu wa Teshome, watuhumiwa watatu walikamatwa kwenye tukio hilo, mmoja wao akiwa mwanamke.
Huu ulikuwa mkutano wa kwanza wa hadhara wa Abiy kwenye mji mkuu huo tangu kuingia madarakani mwezi Aprili, ingawa alishatembelea na kuhutubia maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
"Ethiopia itakuwa ya juu tena, na misingi yetu itakuwa upendo, umoja na ujumuishaji," alisema kwenye mkutano huo wa Jumamosi (Juni 23) akiwa amevalia fulana ya kijani na kofia.
Mageuzi makubwa chini ya Abiy
Ndani ya kipindi hiki cha miezi mitatu, Abiy amefanya mabadiliko makubwa nchini Ethiopia, yakiwemo ya kuubadili mfumo wa vyombo vya ulinzi, kuwaachia huru wapinzani wa kisiasa, kuanzisha hatua za kuelekea uchumi wa soko huria na kutatua mzozo wa miongo miwili kati ya nchi yake na hasimu wake mkuu, Eritrea.
Abiy alichukuwa nafasi ya Hailemariam Desalegn, aliyejiuzulu mwezi Februari kufuatia wimbi kubwa la maandamano ya umma dhidi ya serikali yake yaliyoanza tangu mwaka 2015 na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Licha ya mageuzi anayoyasimamia kuonekana kuungwa mkono na umma, kuna mashaka ya kukubalika kwake ndani ya chama tawala cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF), ambacho makada wake wanajiona kutengwa kando na hatua za waziri mkuu huyu mpya.
Siku ya Ijumaa (Juni 22), kundi la upinzani liitwalo Ginbot 7 lilitangaza kusitisha mashambulizi yake ya silaha kufuatia mageuzi yaliyotangazwa na serikali ya Abiy.
Mwezi uliopita, Ethiopia ilimuachia huru kiongozi wa ngazi za juu wa Ginbot 7, Andargachew Tsige, na pia waendesha mashitaka wakaondoa kesi dhidi ya kiongozi wa kundi hilo, Berhanu Nega, anayeishi nje ya nchi na ambaye tangu mwaka 2009 alikuwa amehukumiwa kifo kwa tuhuma za kupanga jaribio la mauaji.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Sylvia Mwehozi