1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan

Msaada kwa wakimbizi wa Sudan nchini Chad huenda ukasitishwa

Josephat Charo
12 Machi 2024

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, limesema msaada wa chakula kwa mamia kwa maelfu ya wakimbizi wa Sudan nchini Chad, baadhi yao wakikaribia kufa njaa huenda ukasitishwa.

Wakimbizi wa Sudan
Wakimbizi wa Sudan Picha: Mohammad Ghannam/MSF/REUTERS

Tangu mgogoro wa vita ulipozuka Sudan karibu mwaka mmoja uliopita, zaidi ya wakimbizi wa Sudan nusu milioni wamekimbilia Chad kupitia mpaka mrefu wa jangwa na nchi hiyo sasa ni mojawapo ya maeneo muhimu yenye idadi kubwa ya wakimbizi ikiwa na jumla ya wakimbizi zaidi ya milioni moja. Lakini shirika la WFP linasema linapata tabu kuwalisha wote na wengi tayari wanakosa milo.

Takriban nusu ya wakimbizi watoto wa Sudan wa umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na upungufu mkubwa damu mwilini. Mkurugenzi wa WFP nchini Chad Pierre Honnorat amesema wanahitaji wafadhili watoe fedha wazuie hali ya sasa kuwa janga.