MigogoroSyria
Msaada wa kiutu waanza kusambazwa mji wa Kobane, Syria
27 Januari 2026
Matangazo
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kiutu imesema malori 24 yaliyosheheni vyakula, vifaa vya matibabu na mahitaji ya watoto tayari yamepakuliwa na misaada imeanza kutolewa kwa watu.
Shehena hiyo ndiyo msafara wa kwanza wa misaada kuufikia mji huo tangu kuzuka kwa mapigano kati ya pande hizo mbili mapema mwezi huu.
Serikali ya Syria ilianzisha operesheni kubwa ya kuyatwaa maeneo yaliyokuwa chini ya wapiganaji wa kundi la Wakurdi wa SDF wakilenga kulivunja kundi hilo na kulijumuisha kwenye jeshi la taifa.
Maelfu ya watu waliokimbia mapigano walifurika kwenye mji wa Kobane na wiki iliyopita walilalamika kukosa mahitaji muhimu ikiwemo maji na chakula.