Msaada wa kwanza wa kiutu waingia Ukanda wa Gaza
21 Oktoba 2023Mashirika kadhaa ya habari yameripoti taarifa hizo kupitia waandishi wa habari waliopo pande hizo mbili kwa maana ya Misri na Ukanda wa Gaza.
Mkuu wa Misaada ya Kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema ana matumaini "kuwa shehena hiyo itakuwa ni mwanzo wa juhudi endelevu za kupeleka mahitaji muhimu ... kwa watu wa Gaza" na kutahadharisha kwamba "msafara huo wa kwanza haupaswi kuwa wa mwisho."
Duru zinasema mpaka wa Rafah umefungwa tena baada ya malori hayo 20 kupita.
Msafara huo uliobeba msaada wa kiutu unasimamiwa na Shirika la Hilali Nyekundu la nchini Misri, ambalo ndiyo lina jukumu la kuratibu zoezi la kupelekea misaada ya Umoja wa Mataifa.
Shehena hiyo ni ya kwanza tangu kuzuka kwa vita wiki mbili zilizopita kati ya Israel na kundi la Hamas, wanagambo wa kiislamu wanaotawala Ukanda wa Gaza wenye watu wapatao milioni 2.4.
Msaada wa waanza kuingia baada ya shinikizo la kuwanusuru watu wa Gaza
Kivuko cha Rafah ndiyo ujia pekee wa kuingia Gaza ambao hauko chini ya udhibiti wa Israel, ambayo iliridhia kutumwa kwa msaada wa kiutu kutokea Misri baada ya ombi kutoka kwa Marekani, iliyo mshirika mkuu wa dola hiyo.
Israel imekuwa ikiishambulia Gaza kwa makombora tangu kundi la Hamas lilipofanya shambulizi baya kabisa katika historia ya miaka ya karibuni ndani ya ardhi ya Israel.
Shambulizi hilo la Oktoba 7 lilisababisha vifo vya karibu watu 1,400 nchini Israel na mamia wengine kuchukuliwa mateka.
Tangu wakati huo Israel imeweka vizuizi vikali zaidi kwa Ukanda wa Gaza ikisitisha usambazaji wa chakula, maji, madawa na nishati ya umeme pamoja na mafuta.
Israel inasema inataka kulitokomeza kundi la Hamas inalolizingatia kuwa la kigaidi.
Tangu wakati huo kumekuwa na shinikizo la kutaka msaada wa kiutu uruhusiwe kuingia Gaza kuwasaidia mamia kwa maelfu ya watu waliokwama katikati ya mapigano pamoja na watoa huduma za dharura wanaoelemewa kwa idadi kubwa ya majeruhi.
Viongozi duniani wakaribisha kupelekwa msaada wa kiutu Gaza
Viongozi kadhaa duniani wameikaribisha hatua ya kuanza kuingia msaada Gaza. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema "hiyo ni hatua muhimu ya kupunguza madhila kwa watu wasio na hatia"
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesifu taarifa za kuwasili kwa msaada wa kiutu Ukanda wa Gaza akisema ni "habari njema" na kwamba Ujerumani itafanya kazi "kupitia njia zote kuondoa mateso yaliyosababishwa na mzozo huu"
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza James Cleverly amesema kuwasili kwa msaada Gaza hakupaswi kuwa jambo la mara moja na badala yake malori zaidi lazima yaruhusiwe siku zinazokuja.