Msafara wa meli wa kina Greta Thunberg waelekea tena Gaza
31 Agosti 2025
Msafara wa meli zinazobeba misaada ya kibinadamu na wanaharakati, wakiwemo mpiganiaji wa mazingira kutoka Sweden Greta Thunberg, uliondoka mjini Barcelona Jumapili ukiahidi kuvunja "mzingiro haramu wa Gaza,” kwa mujibu wa waandaaji.
Takriban meli 20 zilitoka bandarini katika pwani ya mashariki mwa Uhispania saa 9:30 alasiri (1330 GMT) zikiwa na kauli ya kufungua "njia ya kibinadamu na kumaliza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina,” taarifa ya Global Sumud Flotilla ilisema, neno "sumud” likiwa na maana ya "ustahimilivu” kwa Kiarabu.
Msafara huo, ukipeperusha bendera za Palestina, una mamia ya watu kutoka mataifa mbalimbali, akiwemo muigizaji wa Ireland Liam Cunningham, muigizaji wa Uhispania Eduard Fernandez, wabunge wa Ulaya, na watu mashuhuri wakiwemo aliyekuwa Meya wa Barcelona Ada Colau. Inatarajiwa kufika Gaza katikati ya Septemba.
"Swali hapa leo si kwa nini tunasafiri. Hii si habari kuhusu safari yetu, bali kuhusu Palestina, kuhusu jinsi watu wanavyonyimwa makusudi njia za msingi za kuishi, na jinsi dunia inavyobaki kimya,” Thunberg aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kuondoka.
Cunningham naye aliongeza kuwa hatua ya msafara huu ni ishara ya kushindwa kwa dunia kulinda sheria za kimataifa za kibinadamu, akieleza kuwa ni kipindi cha aibu katika historia ya dunia.
Waandaaji walisema meli nyingine kadhaa zitaondoka Tunisia na bandari nyingine za Mediterania mnamo Septemba 4 kujiunga na msafara huo wa misaada. Aidha, maandamano na kampeni nyingine za mshikamano zitafanyika kwa wakati mmoja katika nchi 44 kote duniani.
'Misheni kubwa zaidi ya mshikamano katika historia'
Thunberg, ambaye ni sehemu ya kamati ya uongozi ya msafara huo, aliandika kwenye Instagram kuwa hii "itakuwa misheni kubwa zaidi ya mshikamano katika historia, ikiwa na watu na meli nyingi zaidi kuliko juhudi zote zilizopita kwa pamoja.”
Hata hivyo, Israel tayari imezuia juhudi mbili za awali za kufikisha misaada Gaza kwa meli mnamo Juni na Julai. Mnamo Juni, wanaharakati 12 kutoka mataifa mbalimbali, akiwemo Thunberg, walikamatwa kilomita 185 magharibi mwa Gaza na hatimaye kufukuzwa. Julai, wanaharakati wengine 21 kutoka nchi 10 walizuiwa walipojaribu kuifikia Gaza kwa kutumia chombo kingine, Handala.
Serikali ya Uhispania imesema itatoa ulinzi wa kidiplomasia na kibalozi kwa raia wake walioko kwenye msafara huo, huku Waziri wa Mambo ya Nje Jose Manuel Albares akithibitisha hatua hiyo Jumamosi. Madrid mwaka jana iliitambua Palestina kama taifa huru.
Hali ya kibinadamu Gaza imeendelea kuzorota wiki za hivi karibuni. Umoja wa Mataifa umetangaza hali ya njaa katika eneo hilo mwezi huu, ukionya kuwa watu 500,000 wanakabiliwa na hali mbaya sana.
Vita vya Gaza vilichochewa na shambulizi lisilokuwa na kifani la kuvuka mpaka la kundi la Hamas nchini Israel mnamo Oktoba 7, 2023, lililosababisha vifo vya watu 1,219, wengi wakiwa raia.
Operesheni ya kulipiza kisasi ya Israel imeua Wapalestina wasiopungua 63,371, wengi wao raia, kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, takwimu ambazo Umoja wa Mataifa unazitambua kuwa sahihi.
Chanzo: afpe