Msafara wa misaada wawasili Syria
11 Januari 2016Msafara wa Umoja wa Mataifa wa chakula na madawa umewasili nje ya mji huo uliozingirwa ukiwa na magari 40 yanayosubiri kuingia.
Msafara huo hautovuka kuingia Madaya hadi hapo msafara sanjari na huo utakapoweza kuingia katika miji miwili ya wakaazi wa Kishia inayoshikiliwa na serikali na kuzingirwa na waasi wa itikadi kali kaskazini magharibi ya Syria.
Duru kutoka chma cha hilali Nyekundu cha Syria imesema takriban tani 330 za msaada wa chakula na madawa zinapelekwa katika mji wa Madaya na unaweza kutumika kwa siku 40.
Mji huo ulioko kama kilomita 25 kaskazini mwa mji mkuu wa Damascus umekuwa ukizingirwa tokea mwezi wa Julai na vikosi vilivyo tiifu kwa Rais Bashar al Assad vikisaidiwa na wanamgambo wa kundi la Hezbollah.
Wakaazi wanakufa njaa
Zaidi ya watu 20,000 hivi sasa wamekwama ndani ya mji huo wa Madaya kwa mijibu wa Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka ambalo limesema watu wengine watano wamekufa njaa wakati wa usiku.
Wiki iliopita shirika hilo limesema watu 23 wamekufa njaa katika hospitali ya mji huo ambayo imekuwa ikiisaidia tokea mwanzoni mwa mwezi wa Disemba.
Vijiji vya Washia vya Foua na Kafraya vilioko kaskazini magharibi mwa jimbo la Idlib vimekuwa vikizimgirwa na waasi tokea mwezi wa April.Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria limesema mtu mmoja amekufa kutokana na uhaba wa chakula na madawa katika vijiji hivyo.
Kukomesha mauaji ya raia
Ikiwa zimebaki kama wiki mbili kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya kutafuta usuluhishi kwa mzozo huo wa Syria waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amezitaka Urusi na Syria kukomesha operesheni zao za kijeshi dhidi ya raia na hususan kukomesha maafa yalioko katika mji wa Madaya na miji mengine iliozingirwa nchini humo kutokana na vituo vya ukaguzi vya serikali.
Fabius amesema "Tumezungumzia umuhimu mkubwa kwa Syria na Urusi kuzuwiya opesheni zao za kieshi dhdi ya raia.Nimetaja miji miwili tu lakini kuna miji mengine na hususan maafa katika mji wa Madaya na miji mengine ya Syria inayozingirwa na vikosi vya serikali kutokana ukaguzi wa vituo vyake."
Shirika la Madaktari wasiokuwa na Mipaka limeonya kwamba usambaazaji wa chakula na madawa katika mji wa Madaya unatakiwa kufanyika kwa kawaida na kwamba mkupuo mmoja wa misaada hiyo hautoshi.
Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa/AP
Mhariri: Mohammed Khelef