1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako dhidi ya watetezi wa haki waendelezwa Iran

5 Septemba 2018

Idara za Usalama nchini Iran zimeongeza kasi ya msako dhidi ya watetezi wa haki za binadamu. Taarifa hiyo imetolewa leo na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch.

Reza Khandan und seine Frau  Nasrin Sotoudeh
Wakili wa Iran Nasrin Sotoudeh pamoja na mumewe Reza KhandanPicha: Getty Images/ B. Mehri

Tangu tarehe 31 mwezi Agosti mwaka huu, maafisa wa usalama waliwakamata watetezi wanne zaidi, pamoja na Reza Khandan, mumewe wakili maarufu wa haki za binadamu ambaye anazuiliwa Nasrin Sotoudeh, wote walio mjini Tehran.

Wakili wake Mohammad Moghimi amesema Khandan alikamatwa mapema leo nyumbani kwake Tehran na maajenti wa Wizara ya Upelelezi nchini Iran. Alihamishwa hadi gereza la Evin Kaskani ya Tehran ambapo  alihukumiwa kwa kushirikiana kwenda kinyume na usalama wa taifa, kueneza propaganda kuhusu mfumo na kuendesha kampeni dhidi ya vazi la kiislamu.

Kosa la kampeni dhidi ya vazi la kiislamu lilitokana na beji zilizopatikana nyumbani kwake zilizokuwa na maandishi ya kupinga ulazima wa wanawake kuvaa hijabu, "No to compulsory hijab". Mkewe Khandan ni mmoja wa wanaharakati maarufu na aliwahi kushinda tuzo za Sakharov la Bunge la Uropa la haki za binadamu mwaka 2012.

Raia wa Iran akiwa ameshikilia Koran wakati wa maandamano kutaka kufufuliwa kwa vazi la kiislamu, hijabu.Picha: Getty Images/AFP/B. Mehri

Mapema mwaka huu, Sotoudeh alijihusisha na kesi nyingi za wanawake waliokamatwa kwa kusimama hadharani bila hijabu, ambayo iliwekwa kuwa lazima nchini Iran baada mapinduzi ya kiislamu ya mwaka 1979. Alikamatwa mwezi Juni na kupatikana na hatia ya kupeleleza mashtaka ya Mahakama ya Mapinduzi ya Tehran.

Mawakili wake wanasema kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka sita, mwaka mmoja zaidi na ilivyoripotiwa awali. Alianza kususia chakula tarehe 25 mwezi Agosti kupinga shinikizo zinazotolewa kwa familia yake. Dhamana ya Khandan ilitajwa kuwa dola elfu hamsini ambayo wakili wake anasema haikubaliki kisheria.

Polisi Iran walaumiwa kwa kuharibu sifa ya nchi

Mkuu wa Shirika la Human Rights Watch katika eneo la Mashariki ya Kati Sarah Leah Whitson amesema kwamba polisi nchini Iran wanaendelea kuharibu sifa yao nchini humo na kimataifa kwa kuendelea kuwazuia mawakili wengi na wanaharakati kwa kuwa wanatetea haki za kimsingi za wananchi. 

´´Katika wakati huu ambapo maisha ya kila siku yanaendelea kuwa magumu kwa mamilioni ya raia wa Iran, wanaharakati wa haki wanafaa kuwa muhimu katika kusuluhisha matatizo ya pamoja, badala ya kuendelezwa kwa msako na serikali.´´

Miongoni mwa  waliokamatwa wiki kadhaa ilizopita ni pamoja na Qasem Sholehsaadi, wakili ambaye alituma ujumbe kupitia video na kusema kwamba atasimama mbele ya bunge la Iran kupinga ukaguzi unaofanywa na Baraza la Usimamizi wa dola, ambalo amelitaja kuwa ndio chanzo cha matatizo ya Iran.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/HRW

Mhariri: Mohammed Abdulrahman