1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako mkali unaendelea Ufaransa

Admin.WagnerD12 Desemba 2018

Msako mkali unaelendelea kaskazini mashariki ya Ufaransa  kumtafuta mshambuliaji mmoja aliyefyetua risasi karibu na soko mashuhuri la Krismasi kwenye mji wa Strasbourg ambapo watu wawili wamekufa na 13 wamejeruhiwa. 

Frankreich Polizeieinsatz nach Schießerei auf dem Weihnachtsmarkt in Straßburg
Picha: Reuters/V. Kessler

Polisi nchini Ufaransa imesema imemtambua mshukiwa aliyetekeleza shambulio hilo na imemtaja kuwa ni Cherif Chekatt mwenye miaka 29, mzaliwa wa mjini Strasbourg ambaye idara za ujasusi zilimuorodhesha kama kitisho kwa usalama.

Mshambuliaji huyo aliyefyetua hovyo risasi kwenye soko la Krismasi mjini Strasbourg ambalo huwa ni kivutio kikubwa kwa maelfu ya watu mwishoni mwa mwaka.

Polisi imesema tayari inawashikilia watu watano kuhusiana na mkasa wa Strasbourg.

Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Laurent Nunez amekiambia kituo kimoja cha radio kuwa msako mkali unaendelea lakini hajaondoa uwezekano kuwa mshukiwa huyo huenda ametoroka na kuondoka kabisa nchini ufaransa.

Mamlaka za ufaransa zimepandisha kiwango cha hali ya tahadhari kufikia cha juu kabisa, ulinzi umeimarishwa zaidi mipakani na wakazi wa mji wa Strasbourg wameombwa kuwa watulivu wakati polisi inaendelea kumtafuta mshambuliaji huyo.

Ujerumani pia imetangaza kuimarisha ulinzi kwenye eneo lote la mpaka wa mto Rhine kuhakikisha mshukiwa huyo anatiwa nguvuni.

Mshambuliaji hajulikani alipo

Picha: Reuters/C. Hartmann

Hadi sasa maafisa wa polisi hawajui alipo na idara za usalama zinatumia kila njia ikiwemo makomando wa kijeshi na helikopta za polisi kumsaka.

Duru za habari zinasema mshambuliaji huyo alikabiliana na polisi kwa kurushiana risasi muda mfupi baada ya kutekeleza shambulio kwenye soko la krismasi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amefanya mkutano wa dharura na baraza lake la mawaziri kufuatia shambulizi hilo.

Kulingana na wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa, polisi inayo rikodi za mshukiwa huyo ambaye alifungwa jela mara kadhaa, karibuni kabisa ikiwa mwaka 2015.

Mwendesha mashatka mkuu wa Ufaransa amesema sababu za shambulio hilo haijafahamika na hakuna kundi lolote la kigaidi lililodai kuhusika.

Meya : Maisha lazima yendelee

Picha: Reuters/C. Hartmann

Meya wa mji Strasbourg Roland Ries amekiambia kituo cha televisheni kuwa cha BFM kuwa maisha lazima yaendelee na kuwataka wakazi wa eneo hilo kuwa imara dhidi ya kitisho cha gaidi mmoja aliyejaribu kuvuruga mtindo wa maisha wa kawaida kwenye mji huo.

Mji wa Strasbourg unazingatiwa kuwa miongoni mwa miji muhimu kwenye kanda ya umoja wa ulaya ukiwa ni moja ya makao  makuu ya Bunge la Umoja huo.

Mapema leo waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa  Christophe Castaner alitangaza kuwa maandamano ya umma yamepigwa marufuku mjini Strasbourg ili kuwapa askari nafasi ya kuendesha msako bila ya kutatizwa na wazazi wameelezwa kuwa wana uhuru wa kuamua iwapo wanataka watoto wao leo kwenda shule au la.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW