Msako wa MH370 waanza tena katika kisiwa cha Reunion
10 Agosti 2015Kwa mujibu wa maafisa wanaosimamia msako huo ndege ya kutafuta mabaki ilizunguka umbali wa kilomita 5,300 za mraba, katika eneo la mashariki ya kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi hata baada ya meli kuondoka kwa kuchelea hali mbaya ya hewa. Japo jua liliangaza vizuri Jumapili, maafisa wa serikali walisema kuwa meli ya jeshi la wanamaji ingelishirikishwa katika shughuli hiyo pale tu chombo chochote kingelionekana baharini.
Msako huo umewavutia wachunguzi wengi, huku mkaazi mmoja akisema huenda ni hatua itakayofanikisha shughuli hiyo huku akionyesha kipande cha bati kwa kwa kejeli na mwingine akidai kutafuta vito vya thamani.
Mwishoni mwa mwezi wa Julai, msako wa ndege hiyo ulipelekea kupatikana kwa bawa moja katika kisiwa hicho cha Reunion, ambacho baadaye waziri mkuu wa Malaysia alithibitisha kipande hicho kilikuwa cha ndege aina ya Boeng 777 iliyotoweka tarehe 8 mwezi machi mwaka 2014 ikiwa na abiria 239.
Ufaransa: hakuna kifaa kipya kilopatikana
Usimamizi wa Malaysia wenyewe ulionekana kutetereka juma lililopita baada ya kutangaza kuwa kiti na dirisha ya ndege hiyo iliyotokomea, vimeonekana huku wachunguzi wa Ufaransa wakisimama kidete kwamba hakuna kifaa kipya kilichoonekana.
Saint Andre, mji uliosemekana kupatikana kwa mabaki hayo umeshuhudia idadi kubwa ya wanahabari katika harakati za kupekua habari zaidi. Hata hivyo, wanahabari hao waliishia kuhudhuria ibada maalum iliyoandaliwa kwa wahanga 239 wa ndege ya MH370. Huku meya wa mji huo akitoa taarifa kwamba, wako tayari kuwapokea jamaa za wahanga hao iwapo wana azma ya kujumuika nao.
Utawala wa kisiwa hicho, pia unatumia ndege ndogo za uchukuzi pamoja na helikopta tatu za polisi na jeshi la wanamaji na boti tatu kusaidia msako huo. Shughuli hiyo hali kadhalika inafanyika nchini Mauritius, ambako serikali ina matumaini ya kupatikana kwa sehemu ya ndege hiyo katika pwani yao.
Sasa ni zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne, tangu ndege ya MH370 inayomilikiwa na shirika la ndege la Malaysia kutoweka ikiwa na abiria 239. Juhudi za kimataifa kutafuta mabaki ya ndege hiyo, zimeongezwa na kuimarishwa japo juhudi hizo hazijafua dafu. Matumaini ya jamaa wa abiria wake yanadidimia kila uchao, huku wakiilaumu Malaysia kwa kutoa taarifa tatanishi juu ya msako huo.
Mwandishi: Ambia Hirsi/Afpe
Mhariri: Mohammed Khelef