Msalaba Mwekundu: Yanayotokea Syria ni vita vya wenyewe kwa wenyewe
17 Julai 2012Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu (ICRC) ni mlezi wa makubaliano ya Geneva ambayo ndiyo yamefafanua sheria za vita na mkataba huo ndio unaotumika kupima ukubwa wa machafuko mpaka kufikia ngazi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Shirika moja la kujitegemea wa masuala ya kibinaadamu ilikwishawahi kuyataja machafuko yanayoshuhudiwa Syria kuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi ya serikali na makundi ya wapinzani yenye silaha hususan katika maeneo ya Homs, Idlib na Hama.
ICRC imezingatia nini hasa?
Lakini uhasama na ghasia zimezidi kuenea nchini humo, na kusababisha shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Geneva Uswisi kuhitimisha kuwa machafuko hayo yamefikia kiwango cha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Shirika hilo limezitaarifu pande hizo mbili zinazogombana kuhusiana na uchambuzi huo na kuzieleza juu ya uwajibikaji wao kwa mujibu wa sheria.
Msemaji wa kamati hiyo ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu, Hicham Hassan, ameliambia Shirika la Habari Reuters kuwa vita vinavyoendelea Syria si vya kimataifa. Na sio kila eneo limeathirika, lakini ghasia hizo haziko katika maeneo hayo matatu tu, zimesambaa katika maeneo mengine pia.
ICRC: Ndiyo Syria inaweza kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita
Tafsiri hiyo inamaanisha kuwa watu wanaoamrisha au kufanya mashambulizi dhidi ya raia yakiwemo mauaji, mateso na ubakaji au kutumia nguvu kubwa dhidi ya maeneo ya raia, wanaweza kushitakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita, kwa kukiuka sheria ya kimataifa.
Kwa miezi 17 ya vita nchini Syria, ICRC ndio shirika pekee la kimataifa lililoweza kutuma wafanyakazi wake wa misaada kuwapa raia chakula, matibabu na mahitaji mengine muhimu katika uwanja wa vita.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Chuo cha Sheria na Haki za Binadamu mjini Geneva, Andrew Clapham, amesema tafsiri ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kuhusiana na machafuko ya Syria ni muhimu.
Ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa uchambuzi huo una maanisha kuwa mashambulizi yanayosababisha watu wengi kupoteza maisha, kujeruhiwa na kuharibu mali yatakuwa ni sawa na uhalifu wa kivita na wahusika wanaweza kufunguliwa mashtaka kutokana na kiwango cha maovu yao.
Katika hotuaba yake tarehe 26 Mwezi uliopita Rais wa Syria, Bashar al- Assad alitamka kwamba nchi yake imo vitani.
Jumamosi iliopita , waangalizi wa Umoja wa Mataifa waliingia katika kijiji cha Tremseh, kilichopo katikati ya Syria, siku mbili baada ya wanaharakati kudai kuwa watu 220 waliuwawa na helikopta ya wanajeshi, hatua iliyozusha ghadhabu kwa mataifa ya nje.
Mwezi Mei, mwaka huu shirika la kimataifa la msalaba mwekundu lilisema waasi wa Syria wanawaklilisha jeshi la upinzani lililojipanga na kutaja juu ya machafuko mjini Homs na Idlib.Baadae Kamati hiyo ya Msalaba Mwekundu ikauongeza mji wa Hama katika orodha yake ya maeneo yenye machafuko ya kiwango cha juu.
Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul
Mhariri:Abdul-Rahman, Mohammed