1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msemaji mkuu wa IS al-Adnani auawa

Yusra Buwayhid31 Agosti 2016

Kundi la wanamgambo wenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu - IS, limethibitisha kifo cha msemaji wake mkuu, Abu Mohamed al-Adnani, aliyekuwa akisimamia operesheni za kijeshi nchini Syria.

Abu Mohammed al-Adnani Pressesprecher Islamischer Staat
Picha: US-Außenministerium

Marekani imesema vikosi vya muungano wa kijeshi vilifanya shambulio la angani lilomlenga Adinani katika jimbo la Aleppo hapo jana, na kwamba bado inatathmini matokeo ya shambulio hilo. Lakini kifo cha kiongozi huyo kimetajwa kitakuwa ni pigo kubwa kwa kundi la IS.

Adnani ni miongoni mwa viongozi wa mwisho wa ngazi za juu wa kundi hilo walio hai, pamoja na mwenzake Abu Bakr al-Baghdadi aliyelianzisha kundi hilo na kuishtua Mashariki ya Kati kwa kuyakamata maeneo makubwa ya Iraq na Syria mnamo mwaka 2014.

Kama msemaji mkuu wa kundi la IS, Adnani alikuwa ni kiongozi aliyeonekana sana hadharani. Na kama kiongozi wa operesheni za za nje kijeshi, jukumu lake lilikuwa ni kupanga mashambulizi ya nje ya Syria, ikiwa ni pamoja na yanayolilenga bara Ulaya. Mashambulizi ya nje yamekuwa ni mkakati muhimu kwa kundi hilo, kutokana na kupoteza nguvu zake za kijeshi nchini Syria na Iraq.

IS yasema kifo cha Adnani si pigo kwao

Chini ya uongozi wa Adnani, kundi la IS lilifanya mashambulizi ya kiwango kikubwa ya kulipua mabomu pamoja na kutumia risasi dhidi ya raia wa nchi kama Ufaransa, Ubelgiji pamoja na Uturuki. Kundi la IS limesema kifo cha Adnani hakitowaumiza, na wameahidi kuwa watu waliomuua watakabiliwa na ilichokitaja kuwa ni "adhabu".

Adnani ametokea Idlib, kusini-magharibi mwa jimbo la Aleppo. Kabla ya kujiunga na kundi la IS aliwahi kulitumikia kundi la al-Qaeda kwa muongo mzima. Kulingana na taasisi ya utafiti ya Brookings, Adnani aliwahi kufungwa gerezani na vikosi vya Marekani nchini Iraq.

Hali ya vita katika jimbo la AleppoPicha: picture-alliance/ZUMA Press

Mchambuzi wa makundi ya kijihadi, Aymenn jawadTamimi, amesmea kifo chake kinaashiria kuanguka kwa kundi hilo la kijihadi.Kifo cha Adnani kimekuja katika wakati ambapo wanamgambo wanaoungwa mkono na Wakurdi kaskani mwa Syria wamekubali pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano ya karibu wiki nzima na vikosi vya Uturuki.

Kwa mara ya kwanza tokea kuanza vita vya Syria miaka mitano iliyopita, Uturuki ilianzisha mashambulizi makubwa ya karibu wiki nzima katika mpaka wake na Syria, na kusema kwamba lengo ni kuwateketeza wanamgambo wa kundi la IS pamoja na wa Kikurdi.

Wapiganaji wa kundi la waasi wa Kikurdi nchini Syria, YPG wamedhibiti maeneo ya kaskazini pamoja na kaskazini-mashariki nchini humo. Na Uturuki ina wasiwasi huenda Wakurdi hao wakajitawala katika eneo hilo jambo litakalowapa nguvu waasi wa Chama cha Wafanyakazi cha Kikurdi cha Uturuki (PKK) kilichopo upande wa pili wa mpaka kusini-mashariki mwa Uturuki.

Mwandishi: Yusra Buwayyhid/afpe/rtre

Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi