1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msemaji wa IDF asema Hamas haiwezi kusambaratishwa

20 Juni 2024

Katika hali isiyo ya kawaida na inayooashiria mpasuko kati ya jeshi la Israel na serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, msemaji mkuu wa jeshi Daniel Hagari amesema Jumatano kuwa Hamas haiwezi kusambaratishwa.

Israel | Msemaji wa IDF Daniel Hagari
Msemaji wa IDF Daniel Hagari amesema Hamas ni itikadi iliyokita mizizi katika nyoyo za watu wa Gaza na siyo rahisi kuishinda.Picha: dts Nachrichtenagentur/IMAGO

Vita vilivyodumu kwa zaidi ya miezi minane vilivyosababishwa na uvamizi usio kifani wa Hamas wa Oktoba 7 dhidi ya Israel vimeshindwa kuwaondoa wapiganaji hao kutoka Ukanda wa Gaza, lakini vimesababisha uharibifu mkubwa.

"Kusema kwamba tutaifanya Hamas itoweke ni kutupa mchanga machoni mwa watu. Ikiwa hatutatoa njia mbadala, mwishowe, tutakuwa na Hamas," Admiral Daniel Hagari alikiambia kituo cha utangazaji cha Channel 13 cha nchini Israel.

"Hamas ni itikadi, hatuwezi kuondoa itikadi."

Soma pia: Netanyahu aishutumu Marekani kwa kuzuia msaada wa silaha

Matamshi yake yalitupiliwa mbali mara moja na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye baraza lake la mawaziri limesisitiza mashambulizi ya Gaza hayatakoma hadi pale Hamas itakaposambaratishwa.

Israel imeendesha vita vya zaidi ya miezi minane yameshindwa kulisambaratisha kundi a HamasPicha: Jim Hollander/UPI Photo/Newscom/picture alliance

"Baraza la mawaziri la kisiasa na usalama linaloongozwa na Waziri Mkuu Netanyahu liliainisha kama moja ya malengo ya vita kuharibu uwezo wa kijeshi na kiserikali wa Hamas," ofisi yake ilisema katika taarifa. "IDF bila shaka imejitolea kwa hili."

Hata hivyo jeshi lilijaribu kutuliza hali kwa kusema katika taarifa kupitia chaneli yake ya Telegram, kwamba Hagari aliizungumzia tu Hamas kama itikadi na kwamba maelezo yake yalikuwa wazi. "Madai mengine yoyote yanaiondoa taarifa hiyo nje ya muktadha."

Shambulio la Oktoba 7 lilichochea vita vya Gaza lilisababisha vifo vya watu 1,194 nchini Israel, wengi wao wakiwa raia, huku kundi hilo likiwachukuwa mateka watu wengine 251, ambapo kati ya hao 116 wanasalia mikononi mwa wapiganaji, ingawa jeshi linasema 41 kati ya hao pia wamekufa. Mashambulizi ya kisasi ya Israel yamewaua watu wasiopungua 37,396 Gaza, pia wengi wao wakiwa raia.

Soma pia: Ripoti: Duru za kijasusi Israel zilionya kuhusu shambulizi la Oktoba 7

Hagari alisema licha ya operesheni iliyowaokoa mateka wanne, yumkini wengi wataachiwa tu kupitia majadiliano.

Hezbollah yazitishia Israel, Cyprus kuhusu mashambulizi ya Lebanon

Hayo yanajiri wakati mzozo mwingine ukizidi kufukuta kati ya Israel na kundi la Hezbollah ambalo limetishia kuwalenga raia wote wa Israel katika vita, baada ya Israel kusema imeidhinisha mipango ya mashambulizi nchini Lebanon.

Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah alisema hakuna mahali patakuwa salama nchini Israeli, katika hotuba iliyotangazwa kupitia televisheni, katikati mwa mvutano mkubwa kwenye mpaka wa Israel na Lebanon.

Nasrallah, ambaye kundi lake lenye nguvu linaloungwa mkono na Iran limeshambuliana karibu kila siku na Israel tangu shambulio la Hamas Oktoba 7, pia alitishia kuilenga Cyprus endapo itaruhusu viwanja vyake vya ndege au vituo vyake kutumiwa na Israel kuishambulia Lebanon.

Kilio cha Waandishi Habari huko Gaza

03:08

This browser does not support the video element.

Kisiwa hicho cha Mediterania kina kambi mbili za kijeshi za Uingereza ikiwa ni pamoja na kambi ya anga, lakini ziko katika ardhi huru ya Uingereza na hazidhibitiwi na serikali ya Cyprus.

Soma pia:Hofu ya vita kamili kati ya Israel na Hezbollah yaongezeka 

Rais wa Cyprus Nikos Christodoulides alikanusha kuhusika kwa nchi yake katika vita hivyo na kusema ni "sehemu ya suluhu", akiashiria jukumu lake katika ukanda wa baharini wa kibinadamu kuelekea Gaza "unaotambuliwa na jumuiya nzima ya kimataifa".

Katika miaka ya hivi karibuni, vyombo vya habari vya Israeli na Cyprus viliripoti mara kwa mara kwamba vikosi maalum vya jeshi la Israeli vilisafiri hadi Cyprus kufanya mazoezi ya mbinu za kukabiliana na ugaidi pamoja na vikosi vya Cyprus.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW