1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MSF: Kipindupindu chatishia janga Congo Mashariki

9 Desemba 2022

Wafanyakazi wa msaada mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameonya juu ya uwezekano wa kutokea janga la kiafya kutokana na ongezeko la kutisha katika visa vya kipindupindu kwenye kambi za wakimbizi wa ndani.

Kongo I Kanyaruchinya Lager für Binnenvertriebene
Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Katika kituo cha kutibu kipindupindu cha mashariki mwa Kongo, dokta Bishikiwabo Irenge, anajaribu kumbembeleza mtoto wa miaka sita ili aweze kunywa.

Mama wa mvulana huyo, Christine Nyiramahigwe, aliliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters, kwamba alilazimika kukimbia nyumbani wakati wa mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi wa kundi la M23 katika mkoa wa Kivu kaskazini.

"Mtoto alikuwa na kipindupindu na alikuwa anatapika usiku mzima. Nilimuangalia, nikaona alikuwa amaechoka sana. Macho yake yalianza kuzama ndani," alisema Christine akiwa kituo cha matibabu.

Watu waliokosa makazi wakitembea karibu na mabanda yao wakitafuta chakula kwa ajili ya familia zao huko Kanyaruchinya, Desemba 5, 2022.Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Hivi sasa Christine anaishi katika kambi ya muda nje ya mji wa Goma, ambako ugonjwa huo unasambaa kutokana na ukosefu wa makaazi na usafi. Maelfu ya watu waliopoteza makaazi yao wanaishi kwenye kambi hizo.

Soma pia: Hatari ya kipindupindu kwa raia wa Congo walioikimbia Goma

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, limesema kati ya Novemba 26 na Desemba 7, wagonjwa 256 wamelazwa katika kituo chake cha matibabu ya kipindupindu eneo la Munigi, karibu na Goma, na kuongeza kuwa theluthi moja ya wagonjwa hao walikuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Zaidi ya watu 177,000 walikuwa wamekwama katika hali mbaya katika eneo la Nyiragongo, kaskazini mwa mji huo, baada ya kuwakimbia waasi wa kundi la M23 waliokuwa wanasonga mbele katika wiki za karibuni.

Soma pia: WHO yaazimia kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu ifikapo 2030

Na kufuatia mvua kubwa wakati wa msimu wa mvua, watu hao waliokosa makaazi walilazimika kuishi katika mabanda yaliyotengenezwa kutokana na matawi ya miti na maturubai.

Congo imekuwa ikipambana na waasi wa M23 inaodai wanafadhiliwa na Rwanda. Rwanda inakanusha madai hayo.Picha: picture-alliance/ dpa

Dokta Bishikiwabo Irenge, ambaye ni mkurugenzi wa kituo kipya cha kutibu kipindupindu kinachoendeshwa na MSF, anasema walishindwa kuwahudumia wagonjwa wote kutoka kambi za wakimbizi na hivyo kulazimika kuunda kitengo kikubwa zaidi.

Soma pia: Usafi ndiyo adui wa Kipindupindu

Kundi la M23 ambalo wapiganaji wake wengi zaidi ni wa jamii ya kabila la Watutsi, lilianzisha tena mapigano mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya kuwa kimya kwa miaka kadhaa na limeteka maeneo makubwa kaskazini mwa mji wa Goma.

Kinshasa inaituhumu Rwanda kuwa nyuma ya uasi huo, jambo ambalo wataalamu wa Umoja wa Mataifa na Marekani wamelithibitisha katika miezi ya karibuni.

Lakini Rwanda inakanusha tuhuma hizo, na kuishtumu Kinshasa kula njama na waasi wa kundi la FDLR, lililoanzishwa nchini DRC baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Chanzo: Mashirika