1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MSF: Majeruhi zaidi ya 20,000 bado wamekwama Gaza

Sylvia Mwehozi
2 Novemba 2023

Shirika la kimataifa la madaktari wasio na mipaka MSF, limesema hii leo kwamba zaidi ya watu 20,000 waliojeruhiwa bado wamekwama ndani ya Ukanda wa Gaza, wakati zoezi la kuwahamisha majeruhi na raia wa kigeni likianza.

Hospitali ya Ahli Arab Gaza
Watoto wa Kipalestina waliojeruhiwa wakikimbizwa hospitali Picha: Abed Khaled/AP/picture alliance

Katika taarifa yake MSF, imethibitisha kuhamishwa kwa "idadi ya watu waliojeruhiwa vibaya" ikiongezea kuwa wafanyakazi wake 22 wa kimataifa waliokuwa Gaza ni miongoni mwa wale waliofanikiwa kuondoka eneo hilo kupitia kivuko cha mpakani cha Rafah. "Hata hivyo, bado kuna zaidi ya majeruhi 20,000 Gaza ambao wana huduma kidogo za kimatibabu kutokana na mzingiro", imesema taarifa hiyo. Shirika hilo limeendelea kutoa wito kwa idadi kubwa zaidi ya watu kuhamishwa, pamoja na kusitishwa kwa mapigano na misaada muhimu zaidi kuruhusiwa kuingia Gaza. Faris Al-Jawad ni mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa MSF na ameongezea akisema kwamba "Na tunaendelea kutoa wito wa usitishaji mapigano. Tunaendelea kutoa wito wa kukomeshwa umwagaji damu. Ni lazima ukomeshwe. Hauwezi kuendelea tena. Na lazima vifaa viingie ili wafanyakazi wetu wa matibabu waweze kutoa huduma muhimu za kuokoa maisha,  ambazo zinahitajika sana kote. "

Wapalestina wenye uraia wa nchi nyingine wakivuka Rafah kuingia MisriPicha: Arafat Barbakh/REUTERS

Raia wa kigeni waondoka Gaza: Mamia ya raia wa kigeni waingia Misri kutokea Gaza

Usiku wa kuamkia leo, kulizuka mapigano makali kati ya wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Hamas kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa pande zote mbili wakati vita hivyo vikiingia siku ya 27 leo.

Vikosi vya al-Qassam, ambalo ni tawi la kijeshi la Hamas, vimeripoti mapigano kaskazini-magharibi mwa eneo la pwani na kusema wapiganaji wake waliwashambulia wanajeshi wa Israel huko na kusini-mashariki mwa Gaza City kwa makombora ya kukinga vifaru.

Kwa upande mwingine, jeshi la Israel limedai kuwaua "dazeni ya magaidi" na kuharibu miundombinu ya Hamas, ingawa halikutoa taarifa yoyote ya vifo vya askari wake katika mapigano ya usiku. Lakini kwa ujumla wanajeshi takribani 16 wa Israel wameuawa tangu nchi hiyo ilipoanzisha operesheini ya mashambulizi ya ardhini katika Ukanda wa gaza siku ya Jumanne.

Soma pia: Mateka wawili waachiwa huru na kundi la Hamas

Kando na hayo, serikali ya Hamas imesema watu 195 wameuawa kwenye mashambulizi ya Israel ndani ya wiki hii katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia. Katika taarifa hiyo, Hamas imesema kuwa "wahanga wa mauaji ya kwanza na ya pili huko Jabalia wanazidi 1,000" wakiwemo "mashahidi na waliojeruhiwa", ikirejelea mashambulizi ya Israel ya Jumanne na Jumatano.

Wapalestina wakitizama mabaki ya jengo lililoharibiwa kambi ya wakimbizi ya JabiliaPicha: Bashar Thaleb/AFP

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anajiandaa kwa ziara ya pili ya Israelikiwa ni chini ya kipindi cha mwezi mmoja. Blinken atawasili Israel kesho Ijumaa na kukutana na maafisa wa ngazi ya juu akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika kuonyesha mshikamano na nchi hiyo lakini pia kusisitiza haja ya kupunguza vifo vya raia wa Kipalestina.

Blinken pia atapitia Jordan, moja ya taifa la Kiarabu ambalo limefufua mahusiano yake na Israel. Lakini jana Jordan ilimwondoa balozi wake kutoka Tel Aviv hadi pale Israel itakapositisha mashambulizi yake Gaza. Blinken pia atafuatilia mazungumzo yatakayoongozwa na Misri na Qatar kuhusu kuachiliwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas.