MSF yaeleza wasiwasi kuhusu hali nchini Sudan Kusini
6 Septemba 2018Wasemaji wa shirika hilo lenye makao yake makuu Mjini Geneva, Uswisi, wamesema mjini Nairobi kuwa idadi kubwa ya raia nchini humo inakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na uhaba wa chakula na maji safi.
Katika kikao na wanahabari, wakuu wa shirika hilo la kutoa misaada ya huduma za matibabu wameonya kuwa shughuli za kupeleka misaada ya dharura katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo zimetatizika kutokana na ukosefu wa usalama nchini humo.
Teresa Murray, naibu mkurugenzi wa shirika hilo anayesimamia shughuli za kutoa misaada, anasema huenda maafa zaidi yakatokea endapo wafadhili na jamii ya kimataifa hawatoingilia kati kuwezesha misaada zaidi kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa ndani.
"Tayari tunaona kwamba kuna tatizo la uhaba wa chakula, na pia kuna majanga mengine yanayowakumba raia – kama vile kusambaa kwa maradhi hatari ya kuendesha na kutapika na Malaria. Na yote haya yanachangia kuangamiza maisha ya wengi."
Aidha shirika hilo la Medecins sans Frontieres limedai kuwa baadhi ya vituo vyake vya kutoa huduma za matibabu vimeshambuliwa na wapiganaji katika siku za hivi karibuni. Wasemaji wameyataja baadhi ya maeneo yaliyoathirika kutokana na mapigano kuwa ni sehemu za Upper Nile kaskazini mashariki mwa nchi miongoni mwa maeneo mengine.
Hofu ya kukatizwa kwa msaada kwa Sudan Kusini
Kuhusu madai kuwa baadhi ya wafadhili huenda wakasusia michango ya kutuma misaada nchini Sudan Kusini, Murray ametoa mwito kwa wafadhili kuzingatia kwa makini matakwa ya raia wa Sudan Kusini na kutositisha misaada ya kibinaadamu kwa nchi hiyo ili kuokoa maisha.
"Kusitishwa kwa michango yoyote ya kutoa misaada bila shaka inaathiri jitihada zetu za kuwasaidia waathiriwa. Itamaanisha kwamba itabidi kuongeza kiwango cha huduma zetu na hilo ni jukumu kubwa."
Itakumbukwa kwamba serikali ya Marekani ilitishia kusitisha msaada wa zaidi ya dola bilioni 3 kwa Sudan Kusini kutokana na kile ilichokitaja kuwa kutofaulu kwa juhudi za kuleta maelewano baina ya viongozi hasimu kwa lengo ya kumaliza vita nchini humo.
Taifa la Sudan Kusini limekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013 kufuatia mzozo uliozuka baina ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar. Maelfu ya watu tayari wamepoteza maisha yao ilhali takriban watu milioni 4 wametoroka makazi yao.
Mwandishi: Reuben Kyama
Mhariri: Josephat Charo