1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji auwa watoto 19, watu wazima wawili Texas

25 Mei 2022

Rais Joe Biden wa Marekani ameelezea fadhaa yake kwa kushindwa na wale wanaotetea umiliki holela wa silaha wakati taifa nchi yake ikiomboleza msiba mwengine wa kuuawa watoto 19 wa skuli ya kati katika jimbo la Texas.

USA Washington | Ansprache Präsident Joe Biden nach Angriff auf Schule in Uvalde
Picha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

"Nilikuwa nimetarajia nikiwa rais nisingelazimika tena kufanya jambo hili. Mauaji mengine ya maangamizi Uvalde, Texas, kwenye skuli ya kati. Watoto wazuri, wasio hatia wa madarasa ya pili, tatu na nne. Na watoto wadogo wangapi wengine walioshuhudia kilichotokea? Kuwaona marafiki zao wakifariki dunia kama kwamba wako uwanja wa vita, Mungu wangu!" Akionekana kama mtu anayelengwalengwa na machozi, Rais Joe Biden alilihutubia taifa usiku wa kuamkia Jumatano (Mei 25), akiwa ndio kwanza amerejea kutoka mkutano wake wa kilele mjini Tokyo, ambako alikutana na mawaziri wakuu wa Japan, India na Australia. 

Huku nyumbani, kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 18, aliivamia skuli ya kati katika mji mdogo wa Uvalde ulio karibu na mpaka wa Marekani na Mexico katika jimbo la Texas, na kuwamiminia risasi na kuwauwa watoto 19 wa skuli hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 500, wengi wao wenye asili ya Kihispania na kutoka familia masikini.

Rais Biden alitumia hotuba hiyo kudhihirisha upinzani wake dhidi ya umiliki ovyo ovyowa silaha na kukemea tabia ya ugoigoi wa Wamarekani kushindwa kupambana na kundi la wale wanaouunga mkono umiliki huo wa silaha.

Wakati wa kuchukuwa hatua ni sasa

Baadhi ya familia zilizopoteza watoto wao kwenye mauaji ya Texas tarehe 24 Mei 2022.Picha: Marco Bello/REUTERS

Biden alisema kama kuna wakati wa kuchukuwa hatua kubadili sheria hiyo, basi ni sasa. "Ni wakati sasa wa kuyageuza maumivu haya kuwa hatua. Kwa kila mzazi, kwa kila raia wa nchi hii. Tunapaswa kumwambia wazi wazi kila mwanasiasa aliyechaguliwa nchini humu kwamba huu ni wakati wa kutenda. Ni wakati kwa wale wanaozuwia ama kuchelewesha sheria ya kudhibiti silaha. Tunapaswa kuwakumbusha kuwa kamwe hatutasahau. Tunaweza kufanya zaidi, tunapaswa kufanya zaidi ya hivi."

Mapema, Gavana Greg Abbott wa jimbo laTexas alimtaja mshukiwa wa mauaji hayo ni Salvador Ramos, kijana wa miaka 18, raia wa Marekani. Maafisa wa Idara ya Usalama wa Umma ya Texas walikiambia kituo cha utangazaji cha CNN kwamba kijana huyo anaaminika kuwa alimpiga risasi bibi yake kwanza kabla ya kuelekea kwenye Skuli ya Kati ya Robb majira ya saa sita mchana, ambako aliingia akiwa amejihami kwa bunduki mbili na mavazi ya kujikinga na silaha. 

Mbali ya Ramos aliyeuawa na maafisa wa usalama, watu wazima wengine wawili waliuliwa na kijana huyo.

Haya ni mashambulizi mabaya kabisa ya aina hii tangu yake ya mwaka 2012, ambapo mshambuliaji aliivamia skuli nyengine ya kati na kuwauwa wanafunzi 20 na wafanyakazi sita. 

Hili ni tukio la 200 kwa mwaka huu pekee ambapo washambuliaji wameshambulia na kuuwa watu hadharani.