Mshambuliaji wa Christchurch afungwa maisha jela
27 Agosti 2020Jaji Cameron Mander amesema hukumu hiyo ambayo ndiyo ya juu zaidi na kwanza ya kutolewa nchini New Zealand inalenga kuonesha jinsi matendo ya mshambuliaji huyo Brenton Tarrant yalivyokosa utu na ubinadamu.
Jaji Mander ameongeza kusema kuwa makosa yaliyofanywa na mwanaume huyo raia wa Australia ni ukatili wa kiwango kibaya ambao hata hukumu ya maisha jela haiwezi kufuta hasara na maumivu aliyosababisha.
Katika mashambulizi ya Machi 2019, Tarrant aliwashambulia kwa bunduki za rashasha waumini waliokuwa kwenye ibada katika msikiti wa Al Noor na Linwoood mjini Christchurch.
Tangu mwezi Machi mwaka huu Tarrant alikubali mashtaka yaliyokuwa yakimkabili. Mshambuliaji huyo alisema anakiri kuwa na hatia ya kuwauwa waumini 51, na jaribio la kuwauwa wengine 40 katika mashambulizi ya bunduki aliyoyafanya mwezi Machi mwaka 2019.
Pia alikiri kuwa na hatia kwa kuhusika katika tendo la kigaidi.
Kisa kilichoshinikiza mageuzi
Kisa hicho kiliutikisa ulimwengu na jamii za watu wa New Zealand ambayo ilifanya mageuzi ya sheria zake na kupiga marufuku umiliki wa bunduki za kivita.
Mtandao wa facebook pia ulitangaza kuwa utatilia mkazo uwezo wa kupeperusha matangazo moja kwa moja baada ya Tarrant kutumia mtandao huo kupeperusha moja kwa moja mashambulizi yake dhidi ya misikiti miwili mjini Christchurch.
Baadaye Ardern na Macron watatoa wito huo wa Christchurch kukabiliana na kusambaa kwa habari za chuki na zinazohusiana na masuala ya kigaidi pamoja na viongozi kutoka Uingereza, Canada, Norway, Jordan na Senegal ambao pia watakuwa mjini Paris.
Mpango huo unanuia kutoa shinikizo kwa kampuni za mitandao ya kijamii ambazo zinakabiliwa na miito zaidi kutoka kwa wanasiasa kutoka kote ulimwenguni kuzuia mitandao yao kutumiwa vibaya.
Hali ilivyokuwa Machi, 2019
Baada ya kutokea shambulizi hilo, mjini Christchurch, New Zealand na duniani kwa jumla kulikuwa na mikesha, sala, kumbukumbu na ujumbe wa mshikamano.
"Tuko pamoja na ndugu zetu Waislamu," ni maneno katika bango kubwa jekundu miongoni mwa maua mengi yaliyowekwa katika sehemu moja katika kile wakaazi waliochosema kuwa ni "mji wa huzuni".
Katika "kanisa kuu la mbao" mjini Christchurch, lililojengwa baada ya tetemeko la ardhi la mwaka 2011 ambalo bado limeweka doa katika mji huo , Dean Lawrence Kimberley aliendesha misa katika kuonesha "mshikamano na jamii ya waislamu."
Mjini Auckland , wakaazi wa jamii zote waliokuwa wakitiririkwa na machozi walisimama wakishikana mikono nje ya msikiti wa Umar kutoa heshima zao.
Katika eneo la bahari ya Tasmin , Waaustralia waliopatwa na mshituko kwamba kitendo kama hicho katika taifa hilo ndugu kimefanywa na mmoja wao, waliapa kutoa msaada wowote ule wanaoweza.