1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji wa sinagogi Ujerumani alielezea azma yake kabla

10 Oktoba 2019

Shirika linalofatilia shughuli za mitandaoni za makundi ya jihadi na sera kali za kizalendo limesema mshambuliaji katika sinagogi la Halle, Ujerumani alichapisha mtandaoni msimamo wake kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi.

Deutschland Synagoge in Halle
Picha: Imago Images/S. Schellhorn

Shirika hilo linalojulikana kama SITE pamoja na vyombo vya habari vya Ujerumani, vimesema mshambuliaji huyo mwenye silaha aliyewaua watu wawili kwenye mji wa Halle, mashariki mwa Ujerumani alichapisha mtandaoni azimio linaloelezea msimamo wake kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi wiki moja iliyopita.

Mkurugenzi wa SITE inayofuatilia pia makundi ya uhalifu wa chuki, Rita Katz ameandika katika ukurasa wa Twitter kwamba nyaraka, ambazo ni dhahiri zinaonyesha azimio la mtuhumiwa huyo zimeonekana mtandaoni zikionyesha picha za silaha na risasi alizotumia. Pia zilionyesha lengo lake la kuwaua raia wa kigeni wakiwemo Wayahudi.

Gazeti la Ujerumani la Die Welt limeripoti kuwa nyaraka hizo zenye kurasa 10 zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza na zinataja hasa mpango wa kulishambulia sinagogi la Halle kwenye jimbo la Saxony-Anhalt wakati wa sikukuu takatifu ya Wayahudi ya Yom Kippur.

Mji wa Halle unavyoonekana baada ya shambuliziPicha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Mtandao wa Twitch umesema shambulizi hilo lililotokea jana kwenye mji huo wa mashariki mwa Ujerumani lilionyeshwa mubashara na mshambuliaji kwa dakika 35 katika mtandao wake na limeangaliwa na watu wapatao 2,200 kupitia mtandao huo.

Polisi wamemkamata mtuhumiwa huyo raia wa Ujerumani Stephan B baada ya majibizano ya kurushiana risasi iliyosababisha ajeruhiwe. Kwa mujibu wa maafisa wa usalama, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 hajawahi kukamatwa kabla, lakini uchunguzi wa awali unaonesha ana msimamo mkali kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi na raia wa kigeni na inaonekana alipanga shambulizi hilo peke yake.

Viongozi walaani shambulizi

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Horst Seehofer amesema chuki dhidi ya Wayahudi bila shaka ilikuwa ni lengo la mshambuliaji.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameelezea kusikitishwa na shambulizi hilo ambalo liliwajeruhi pia watu wawili. Jana usiku, Merkel alishiriki katika ibada ya kuwakumbuka wahanga, nje ya Sinagogi jipya mjini Berlin katika kuonyesha mshikamano. Merkel amesema Ujerumani inapinga aina yoyote ya chuki dhidi ya Wayahudi.

Rais wa Baraza Kuu la Wayahudi nchini Ujerumani, Josef Schuster amesema shambulizi hilo la kikatili limewashtua Wayahudi wote wa Ujerumani.

Mishumaa na maua ikiwekwa kuwakumbua waliouawa HallePicha: Reuters/F. Bensch

''Namshukuru Mungu mshambuliaji hakufanikiwa kuingia ndani ya sinagogi kwa sababu ya mitambo ya kiusalama. Lakini polisi hawaweki doria wakati wa sikukuu za Wayahudi, wakati wa ibada za misa makanisani na kwenye vituo vya Wayahudi. Kama polisi wangeweka ulinzi Halle, wangefanikiwa kumzuia mhalifu asilete madhara na asingepata wazo la kushambulia kwenye mkahawa wa Kituruki,'' alisema Schuster.

Viongozi wa makanisa ya Katoliki na Kiprotestanti wametoa salamu za pole na wamewataka watu wa imani zote kupinga chuki dhidi ya Wayahudi.

Bunge la Ulaya lilisimama kimya kwa dakika moja kuwaombea wahanga wa shambulizi hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani shambulizi hilo akisema ni janga jingine baya kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi na kwamba maeneo ya kuabudu duniani yanapaswa kuwa sehemu salama kwa ajili ya kueneza amani na sio kumwaga damu na kufanya vitendo vya kigaidi.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema shambulizi la Halle linadhihirisha tena chuki dhidi ya Wayahudi barani Ulaya.

Balozi wa Marekani nchini Ujerumani, Richard Grenell amesema raia 10 wa Marekani walikuwa ndani ya sinagogi hilo lililokuwa na watu 70 hadi 80.

(AFP, AP)