1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji wa Vienna alikuwa mfuasi wa itikadi kali

4 Novemba 2020

Kansela wa Austria Sebastian Kurz ametoa wito wa kuwepo hatua za pamoja za Ulaya kukabiliana na kile alichokitaja kuwa "siasa za kiislamu" wakati uchunguzi unaendelea kuhusiana na shambulizi la kigaidi la mjini Vienna. 

Österreich Wien nach dem Terroranschlag | Bundeskanzler Sebastian Kur
Kansela wa Austria Sebastian Kurz Picha: Georges Schneider /photonews.at/imago images

Katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Die Welt Kansela Kurz amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kuongoza mapambano dhidi ya siasa za itikadi kali ya dini ya kiislamu alizosema zinaleta kitisho kwa tamaduni na mwenendo wa maisha ya Ulaya.

Kurz amelaani shambulizi la mjini Vienna na kulitaja kuwa "shambulizi la kigaidi lenye kuudhi" ambalo mshambuliaji aliwauwa mhudumu wa mkahawa, mpita njia, mwanaume mmoja mzee pamoja na mwanamke.

Serikali ya Kurz inatarajiwa kuandamwa na maswali juu ya ni vipi mtu mmoja aliyefahamika na vikosi vya usalama alifanikiwa kununua silaha na kutekeleza shambulizi baya kabisa kwenye mitaa ya mji mkuu, Vienna, unaojulikana kwa utulivu na maisha ya fahari.

Ulinzi umeimarisha mjini Vienna Picha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya ndani ya Austria Karl Nehammer, amehimiza kuwepo utulivu wakati uchunguzi unaendelea kutafuta ukweli wa kilichotokea na kusisitiza kuwa ugaidi hautoigawa nchi hiyo.

 "Ugaidi hautoigawa jamii yetu. Ningependa kutaja mfano moja chanya katika kisa hiki: afisa wa polisi aliyejeruhiwa aliokolewa na raia wawili wa Austria wenye historia ya kuwa wahamiaji" alisema Nehammer.

Mapema jana serikali ya Austria ilisema mshambuliaji aliyehusika na kisa cha mjini Vienna alikuwa mfuasi wa kundi linalojiita dola la kiislam, IS.

Mshambuliaji aliwahi kuhukumiwa kifungo gerezani 

Kwa mujibu wa wizara wa Mambo ya ndani,  kijana huyo Kujtim Fejzulai aliyekuwa na umri wa miaka 20, alishatiwa hatiani mwaka uliopita kwa kujaribu kusafiri kwenda Syria kwa lengo la kujiunga na kundi la IS.

Maombolezo yanaendelea Austria kutokana na vifo vya shambulizi la mjini Vienna Picha: Leonhard Foeger/REUTERS

Fejzulai,  ambaye alikuwa na uraia pacha wa Macedonia na Austria alihukumiwa miezi 22 jela lakini alitolewa kwa msahama chini ya utaratibu wa kurekebisha tabia Disemba iliyopita

Fejzulai aliuwawa na polisi muda mfupi baada ya kutekeleza shambulizi hilo na alikutwa akiwa na bunduki ya rashasha, bastola na mkanda bandia wa mabomu. 

Katika tukio hilo washambuliaji kadhaa ikiwemo Fejzulai walifyetua hovyo risasi katikati ya mji Vienna na kusababaisha vifo vya watu wanne, kujeruhi wengine zaidi ya 20 na kuzusha taharuki kubwa.

Hata hivyo Waziri Nehammer amesema hata baada ya kuchunguza picha za video kutoka kamera za kufuatilia nyendo wameshindwa kugundua ushahidi wa kuwepo mshambuliaji wa pili.

Polisi imewataka wale waliorikodi tukio hilo kutuma picha na video kwa mamlaka za Aia ili kusaidia kubaini njia aliyotumia mshambuliaji kuingia katikati ya mji.