1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshauri wa Umoja wa mataifa ataka mzozo ukomeshwe

9 Desemba 2015

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya halaiki amesema ikiwa mzozo nchini Burundi hautakomeshwa huenda kukatokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Pierre Nkurunziza
Picha: I.Sanogo/AFP/GettyImages

Adama Dieng amewaambia waandishi wa habari kuwa anaitumia siku ya kwanza ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji ya halaiki hivi leo (Jumatano tarehe 9 Disemba) kuitaka serikali ya Burundi na upinzani kumaliza mapigano na kujadili jinsi ya kupata suluhisho la kisiasa ili kuleta amani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Dieng amesema anatoa mwito kwa nchi jirani kama Rwanda na Tanzania ambazo zimepokea idadi kubwa ya wakimbizi wanaotoroka mapigano hayo kuisaidia Burundi.

Uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu na baadaye kushinda uchaguzi uliokumbwa na utata umezua mapigano kwa miezi kadhaa sasa, likiwemo jaribio la mapinduzi lililoshindwa. Zaidi ya watu 240 wameshauawa tangu mwezi Aprili na karibu 215,000 wametorokea nchi jirani, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Burundi ina historia ya mapigano kati ya makundi ya kikabila ya Wahutu na Watusti. Nkurunziza aliingia madarakani mwaka 2005 wakati wa kumalizika kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha vifo vya watu 300,000 kati ya mwaka 1993 na 2006.

Maafisa wa polisi wakati wa maandamano ya kupinga awamu ya tatu ya Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Umoja wa Mataifa wapata hofu

Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Raad al-Hussein, amesema hali nchini Burundi ni hatari sana.

"Tunasikitishwa na maneno tu bila hatua yoyote na kuwepo mauaji yanayoelekea kuwa ya kikabila, na hili ni jambo ambalo sisi na nchi katika eneo hili tunalihofia sana," alisema Zeid Raad al-Hussein.

Zeid amesema mashambulizi dhidi ya raia yanaonekana kuongezeka na hii ina maana kuwa pande husika zina lengo la kuzua fujo.

Ikiwa kutakuwa na hali ya utulivu, amesema vijana wa chama kinachotawala sharti waweke chini silaha na kikosi cha polisi cha upelelezi sharti kidhibitiwe. Amesema ni kwa hatua hiyo tu ndipo makundi mengine yaliyo na silaha yataacha silaha zao.

Umoja wa Ulaya wavunjwa moyo

Umoja wa Ulaya umesema huenda ukabana uhusiano wake na Burundi na kusalia kutoa msaada tu baada ya mazungumzo kushindwa kupata suluhisho la tatizo la kaki za kinadamu katika taifa hilo.

Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo ya muda mrefu mjini Brussels ilisema Umoja wa Ulaya ambao ni mfadhili mkubwa wa nchi hiyo ya Burundi unazingatia hatua ambazo Burundi inachukua, lakini hatua hizo huenda sio suluhisho.

Muungano huo umesema itakuwa bora ikiwa serikali itakubali kuzungumza na upinzani. Mazungumzo ya siku ya Jumanne yalifanyika chini ya mkataba wa Cotonou, ambao ni uhusiano wa kiuchumi na maendeleo wa mataifa 28 ya Ulaya pamoja na mataifa ya Afrika, Caribbean na Pacific na ambao umeweka masharti makali ya ushirikiano ikiwemo kuhakikisha haki za kibinadamu.

Mwezi uliopita Ubelgiji, ambayo ilikuwa mkoloni wa zamani wa Burundi, iliwaambia raia wake kuondoka nchini humo huku Umoja wa Ulaya ukiziondoa familia za wafanyakazi wake baada ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa huenda Burundi ikatumbukia kwenye mauaji ya halaiki.

Mwandishi: Bernard Maranga/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef