1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchango wa Ujerumani

18 Novemba 2015

Mshikamano wa walimwengu dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa dola ya kiislam IS na jinsi kitisho cha kutokea mashambulio ya kigaidi kinavyovuruga maisha ya kawaida ya raia ni miongoni mwa mada magazetini

Polisi ya Ufaransa yamsaka muasisi wa mashambulio ya Paris katika kitongoji cha Saint Denis mjini ParisPicha: Reuters/J. Naegelen

Tuanzie lakini na mshikamano wa kimataifa katika juhudi za kuwavunja nguvu magaidi wa IS.Magazeti yote ya humu nchini yameripoti kuhusu wito wa rais wa Ufaransa Francois Hollande kwa washirika wa Umoja wa Ulaya pamoja na jibu la dhati la umoja huo kuisadia Ufaransa katika vita dhidi ya IS.Gazeti la "Volksstimme" linaandika:"Kitu kinachoziounganisha nchi za magharibi,Urusi na washirika wa mashariki ya kati katika mzozo wa Syria ni juhudi za kuliteketeza kundi la magaidi wa dola ya kiislam-IS.Rais wa Ufaransa Francois Hollande aliyesimama kidete baada ya mashambulio ya Paris ijumaa iliyopita anapanga sio tu kuzungumza na rais Barack Obama wa Marekani,bali pia na rais Vladimir Putin wa Urusi kutathmini mkakati utakaosaidia kuwateketeza wanamgambo hao wa kigaidi.Katika hali hii idara ya upelelezi ya Urusi inasema shambulio dhidi ya ndege ya abiria ya nchi hiyo iliyodunguliwa katika anga ya Sinai nchini Misri,lilikuwa la kigaidi.Yadhihirika kana kwamba mambo yamebadilika.Putin anataka pawepo mshikamano wa kimataifa dhidi ya magaidi wa IS.Na wakati haujawahi kuwa muwafak kama hivi sasa.

Msaada wa Ujerumani kwa Ufaransa

Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung linachambua mshikamano huo na kujiuliza jinsi jeshi la shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Bundeswehr litakavyoweza kuchangia.Gazeti linaandika:"Ndo kusema wanajeshi wa Ujerumani watakwenda kupigana nchini Syria?Uwezekano mkubwa zaidi unakutikana pengine kwa wanajeshi wa Ujerumani kwenda Mali kuwapunguzia mzigo wafaransa.Kadhia ya IS si ya Ulaya magharibi tu.Wafuasi wa itikadi kali wameidengua pia ndege ya abiria ya Urusi.Hivi karibuni wameporomosha mabomu na kuwauwa maamia ya watu nchini Uturuki na Libnan.Mshikamano dhidi ya IS hata hauna haja ya kubembelezwa,umejiunda wenyewe.Cha kusikitisha ingekuwa kama rais Francois Hollande angeahidiwa msaada mkubwa zaidi na rais Obama wa Marekani na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kuliko na Umoja wa Ulaya.Msaada wa Ujerumani hapo utatuwama zaidi katika kutoa ushauri,kusisitiza haki za binaadamu ziheshimiwe na kuwatakia kila la kheri wafaransa.Uwezekano huo upo.

Vitisho visitutishe

Na hatimae tunamulika jinsi vitisho vya kutokea mashambulio ya kigaidi vinavyoathiri maisha ya kila siku ya jamii.Gazeti la "Volksstimme" linaandika:"Wajerumani na mashabaiki wa soka walitaka kuteremka katika uwanja wa dimba wa HDI mjini Hannover kubainisha hawatishiki kwa vitisho vya kigaidi.Wakaazi wa Hannover tayari walikuwa wameshajipanga kandili mikononi na nyimbo ya taifa ya Ufaransa-La Marseillaise midomoni kabla ya kipenga cha mwanzo kulia.Walitaka kuonyesha mshikamano wa dhati dhidi ya mashambulio ya Paris kwa Mchuano wa dimba kwaajili ya amani.Hapa nchini na kote ulimwenguni.Kwamba mwishoe vitisho vya shambulio la kigaidi vimepelekea mchuano huo kati ya Ujerumani na Uholanzi kuakhirishwa ni jambo linaloeleweka.Licha ya masikitiko,watu wamedhihirisha moyo wa kupenda amani na mshikamano-wamebeba kandili na bendera ya Ufaransa .Angalao wamejaribu na hilo nalo pia ni muhimu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW