1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUingereza

Mshikamano wa jamii wazima njama za wafanya fujo Uingereza

8 Agosti 2024

Polisi ya London nchini Uingereza imesema kuwa hali iliyoimarishwa wa ulinzi na umoja uliooneshwa na jamii za nchini vilizuia marudio ya vurugu kali zilizoshuhudiwa katika siku za karibuni.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya wageni nchini Uingereza
Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya wageni nchini Uingereza.Picha: Burak Bir/Anadolu/picture alliance

Vurugu hizo zilihusisha mashambulizi ya kibaguzi yaliyowalenga Waislamu na wahamiaji kutokana na kisa cha mauaji ya wasichana watatu mnamo Julai 29 katika shambulizi la kisu mjini Southport.

Makundi ya mrengo mkali yanayopinga uhamiaji yalipanga maandamano kote Uingereza jana.

Katika kujibu, maelfu ya polisi na waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi walijitokeza katika miji ya Uingereza ikiwemo London, Birmingham, Bristol na Newcastle.

Kamishna wa Polisi ya London Mark Rowley amesema kulikuwepo na amani jana usiku isipokuwa tu matukio machache ya uhalifu.

Amewashukuru polisi pamoja na mshikamano uliooneshwa na jamii mbalimbali ili kuzikabili changamoto zilizojitokeza.