1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshikamano wa Ulaya watakiwa kupambana na Virusi vya Corona

26 Machi 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajaribu kuunganisha nguvu zao katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona, ambao tayari unaonekana kuanza kuyumbisha uchumi wa Umoja huo

EU-Staaten einigen sich im Kampf gegen Coronavirus
Picha: picture-alliance/dpa/European Commission/E. Ansotte

Mamilioni ya raia wa Umoja wa Ulaya wanaendelea kuishi chini ya vizuzi vilivyowekwa na serikali zao, kama tahadhari ya kuzuwia kuenea kwa virusi vya Corona  vilivyowauwa zaidi ya wakaazi 10,000 wa Umoja huo, hasa nchini Italia, Ufaransa na Uhispania. 

Hivi karibuni nchi wanachama wa Umoja huo zimekuwa zikichukua hatua za kufunga mipaka yake, kuzuwia kusafirisha madawa na kutumia fedha nyingi bila ya kuzingatia kanuni za umoja wa Ulaya.

Akizungumza mbele ya bunge la Ulaya rais wa halmashauri kuu ya Umoja huo Ursula Von der Leyen  amesema wakati Ulaya ilipohitajika kusaidiana kila nchi iliangalia masilahi yake binafasi.

Ursula ambaye ni waziri wa zamani wa ulinzi wa Ujerumani amesema kwa sasa anajaribu kuunda mpango wa pamoja wa kukabiliana na virusi vya Corona na viongozi wataujadili mpango huo kupitia mkutano utakaofanyika pia kwa njia ya video.

Mfalme Salman asema janga la Corona linauathiri uchumi wa dunia

Picha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Huku hayo yakiarifiwa mfalme Salman wa Saudi Arabia amewahimiza viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi G20 kuchukua hatua za pamoja  kukabiliaana na janga hilo la kidunia na pia kuwataka kutoa msaada kwa mataifa yanayoendelea.

Akiufungua mkutano wa G20 ulifanyika pia kwa njia ya Vidio, Salman amesema janga hilo la Corona linauathiri uchumi wa dunia, masoko ya fedha pamoja na biashara huku akitoa wito wa dunia nzima kuungana pamoja kukabiliana na virusi hivyo. Haya yanajiri wakati virusi hivyo vikiendelea kusambaa kwa kasi duniani.

Nchi tajiri kama Marekani zimetangaza mipango ya mabilioni ya dola ya kuupiga jeki uchumi, lakini bado hakuna hatua zozote za pamoja zilizotangazwa na kundi la G20, ambazo zimekuwa zikikosolewa kwa kujivuta katika kutafuta suluhisho

Haya yanajiri wakati virusi hivyo vikiendelea kusambaa kwa kasi duniani. Uhispania imerekodi leo ongezeko la vifo vitokanavyo na virusi vya Corona baada ya siku 12 ya wakaazi wake kushauriwa kukaa ndani. Hii leo mchana maambukizi mapya yalifikia 8,500 na kufikisha idadi jumla kupindukia watu elfu 56 walioambukizwa huku vifo vikipindukia 4000.

Marekani nayo inaendelea kulemewa kufuatia watu milioni 3.3 kuomba msaada wa serikali kufuati wengi wao kukosa kwenda kazini kufutia mripuko wa virusi vya Corona: Wizara ya kazi nchini humo imesema hiki ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa cha watu wanaoomba msaada wa serikali tangu mwaka 1982 ambayo idadi ya walioomba msaada huo ilifikia watu 695,000

Virusi vya Corona bado vinaendelea kuihangaisha dunia huku watu zaidi ya laki mbili wakipoteza maisha na wengine 471,000 wakiambukizwa virusi hivyo.

Vyanzo: dpa, reuters,afp,ap

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW