1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Dunia yampongeza mshindi wa Tuzo ya Amani Nobel 2024

Hawa Bihoga
11 Oktoba 2024

Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2024 iliyotolewa kwa Nihon Hidankyo, shirika la Kijapani linalowakilisha waathirika wa mabomu ya atomiki, imepokelewa kwa hisia kali kimataifa. Salamu za pongezi zimeendelea kumiminika.

Kamati ya Tuzo ya Amani ya Nobel
Kamati ya Tuzo ya Amani ya NobelPicha: Christine Olsson/TT/picture alliance

Mjini Hiroshima, manusura kama Tomoyuki Mimaki walielezea mshangao na furaha, wakionesha mapambano ya muda mrefu ya kutambua juhudi zao.

Viongozi wa Ulaya, kama Ursula von der Leyen, wamesisitiza umuhimu wa ujumbe huu wakati vitisho vya nyuklia vinaendelea katika mizozo ya kimataifa, hasa nchini Ukraine.

Duniani kote, tuzo hii imeonekana kuwa ukumbusho muhimu wa athari za kutisha za vita vya nyuklia, hasa katika muktadha wa mvutano wa kisiasa unaoongezeka.

Kazi ya Nihon Hidankyo inachukuliwa kama ishara yenye nguvu ya umuhimu wa kudumisha marufuku dhidi ya matumizi ya silaha za nyuklia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, katika salaam zake za pongezi kwa mshindi huyo, amesema manusura wa mabomu ya atomiki kutoka Hiroshima na Nagasaki, ambao wanajulikana kama Hibakusha, ni mashahidi wa kipekee wanaotoa ushuhuda wa gharama za kibinadamu zinazotokana na silaha za nyuklia.

Soma pia:Shirika la Japan lashinda Tuzo ya Amani ya Nobel

Aliendelea kusisitiza kwamba silaha za nyuklia bado zinabakia kuwa kitisho cha wazi kwa ubinadamu, hasa kwa kuzingatia jinsi zinavyoendelea kujadiliwa katika mahusiano ya kimataifa.

Guterres alitoa wito kwa viongozi wa dunia kuona silaha za nyuklia kama zilivyo: "vifaa vya kifo" visivyoleta usalama au ulinzi​.

Mbali na Guterres, viongozi wengine na taasisi kadhaa wametoa maoni yao kuhusu Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2024 iliyotolewa kwa Nihon Hidankyo.

UN: Utambuzi huu ni wa msingi

Msemaji wa ofisi ya kamishna mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Matifaiya Ravina Shamdasan amesema huo ni utambuzi wa msingi hasa kwa manusura ambao wamefanyakazi bila kuchoka.

''Ni utambuzi muhimu sana kwa mashirika ya mashinani na haswa walionusurika na ukiukaji wa kutisha kwa kazi yao ya bila kuchoka na endelevu,"

Shamdasan aliongeza kwamba si kila wakati walikuwa na rasilimali za kutosha katika kuendesha shughuli zao.

"Wanarasilimali za kutosha, lakini wamejaribu kuifanya dunia kuwa pahala salama kwa ajili yetu sote.''

Mwanaharakati wa Iran Narges ashinda tuzo ya Nobel 2023

02:36

This browser does not support the video element.

Jørgen Watne Frydnes, mwenyekiti wa Kamati ya Nobel ya Norway, amesema Hibakusha wametoa ushuhuda muhimu kuhusu mateso na maafa ya silaha za nyuklia, akibainisha kuwa tuzo hii inatolewa wakati ambapo "marufuku dhidi ya matumizi ya silaha za nyuklia iko hatarini."

Soma pia:Mpalestina atunukiwa Tuzo Mbadala ya Nobelmatumizi ya nyuklianobel

Ursula von der Leyen, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, amesema kupitia mtandao wa X kwamba kivuli cha mabomu ya Hiroshima na Nagasaki bado kinatishia ubinadamu.

Aliitaja kazi ya Nihon Hidankyo kuwa yenye thamani kubwa katika ulimwengu wa sasa, akisema kuwa tuzo hii ina ujumbe wenye nguvu kwamba tunawajibika kuwalinda vizazi vijavyo dhidi ya vitisho vya vita vya nyuklia.

Waziri Mkuu wa Japan, Shigeru Ishiba, amesema tuzo hiyo ni ya maana sana, hasa wakati huu ambapo mvutano wa kimataifa, ikiwemo vita vya Ukraine na mzozo wa Mashariki ya Kati, umeongeza hofu kuhusu uwezekano wa matumizi ya silaha za nyuklia.

Ishiba alitambua kuwa tuzo hiyo ni "muhimu sana" ikizingatiwa lengo la shirika hilo na hali ya sasa duniani.