1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshirika wa Rais wa Korea Kusini akamatwa kwa ufisadi

20 Novemba 2016

Waendesha mashitaka nchini Korea Kusini wanasema wanaamini Rais Park Guen-hye alikula njama na mshirika wake mkubwa, ambaye alitumia mafungamano yake na rais huyo kujipatia utajiri mkubwa usiokuwa na maelezo.

Südkorea Park Guen-hye
Picha: picture alliance/AP Photo/B. Seung-yul

Taarifa hizi zinakuja wakati waendesha mashitaka hao wakimtia hatiani rasmi rafiki na mshirika huyo wa muda mrefu wa Rais Park, Choi Soon-sil, kwa tuhuma za kuingilia masuala ya kiserikali na kuzilazimisha kampuni kutoa mamilioni ya dola kwa mifuko aliyokuwa akiiendesha. 

Siku ya Jumapili (Novemba 20), waendesha mashitaka pia waliwatia hatiani wasaidizi wengine wawili wa zamani wa Rais Park, ambao wanashukiwa kushirikiana na Choi katika njama hizo. Choi mwenyewe ni binti wa kiongozi wa kundi moja la kidini, ambaye kabla ya kifo chake alikuwa akimfundisha Rais Park na ambaye alikuwa akimchukulia kama "shujaa" wake. 

Huenda Rais Park akahojiwa na waendesha mashitaka siku chache zijazo. Kiongozi huyo wa kwanza mwanamke wa Korea Kusini amekuwa akikabiliwa na ukosoaji mkubwa, akidaiwa na wapinzani wake kuwa anaihujumu demokrasia. 

Upinzani wataka Park ajiuzulu

Choi Soon-sil (katikati) amefunguliwa rasmi mashitaka ya ufisadi kwa kujipatia na kuzitumia nyaraka za serikali kwa maslahi binafsi licha ya kuwa yeye hana nafasi yoyote serikalini.Picha: Reuters/Seo Myeong-gon

Upinzani, ambao unaungwa mkono na maelfu ya waandamanaji, unamtaka awachie madaraka. 

Polisi inasema maandamano ya siku ya Jumamosi (Novemba 19) yalihudhuriwa na watu 170,000 karibu na Baraza la Mji na lango kuu la kasri kwenye mji mkuu, Seoul, ingawa waandaaji wa maandamano hayo wanasema waliohudhuria ni watu 500,000. 

Waandamanaji wengine walipita kwenye mitaa iliyo karibu na ofisi za rais, huku wakibeba mishumaa na kuwasha simu zao, wakipiga mayowe: "Park Guen-hye achia madaraka" na "Mkamateni Park Guen-hye!"

Mbali na kashfa ya kujipatia na kutumia nyaraka za siri za serikali kujinufaisha binafsi, Choi anatuhumiwa pia kutumia ukaribu wake na Rais Park kuwapatia watoto wake elimu ya juu kinyume na taratibu. Siku ya Ijumaa, Wizara ya Elimu ya nchi hiyo ilikitaka Chuo Kikuu cha Wanawake cha Ewha kumfutia usajili binti wa Choi aitwaye Yoora Chung, baada ya kugundua kuwa chuo hicho kilikiuka taratibu zake katika kumpokea binti huyo.

Hapo Alhamisi, upinzani ulitumia wingi wao bungeni kupitisha sheria ambayo inamruhusu mwendesha mashitaka maalumu kuchunguza kashfa zinazomuandama Rais Park na kuyaweka hadharani maovu yaliyotendwa na kiongozi huyo. 

Kuna uwezekano mkubwa wa bunge kuchukuwa hatua za kumuondosha madarakani rais huyo, kwa vile mwenyewe haonekani kuwa yuko tayari kujiuzulu na, hivyo, kujiondolea kinga ya kutoshitakiwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP,Reuters
Mhariri: Bruce Amani

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW