Mshtuko katika masoko ya fedha duniani
16 Septemba 2008Baada ya jana kuitwa jumatatu nyeusi, kwa vile bei za hisa za makampuni duniani ziliporomoka sana, mabenki ya Kimarekani na masoko ya fedha ya kimataifa leo bado yako katika hali ya wasiwasi na mshtuko. Wawekezaji hapa Ulaya leo wako hamkani wakingojea vipi mambo yanavokwenda katika masoko ya hisa ya Marekani na uamuzi wa Benki Kuu ya Marekani kuhusu vima vipya vya riba kwa ajili ya mikopo. Wakati huo huo, mkuu wa Shirika la Fedha Duniani, IMF, amesema mzozo wa sasa wa fedha duniani haujesha na mabenki zaidi yataweza kufilisika na kufungwa, huenda ikapelekea kutoweka mabenki huru ya uwekezaji.
Mambo si mazuri hata kidogo hivi sasa katika masoko ya fedha duniani. Mtetemeko wa jana katika masoko ya hisa huko NewYork ulikuwa mkubwa kabisa kuwahi kuonekana tangu yalipotokea mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, miaka saba iliopita huko Marekani. Wanasiasa na wakuu wa benki kuu za nchi mbali wanajitahidi kuutuliza wasiwasi ulioko kama mzozo huu utakuwa mbaya zaidi na kutoweza kudhibitiwa.
Na kama ilivyo kawaida ya wanasiasa, Rais George Bush alijaribu kuwatuliza Wamarekani kwa kusema hivi:
"Tutajitahidi kupunguza vurugu na kulainisha athari ya hali hii ilioko katika masoko ya fedha juu ya uchumi wote. Kwa muda mfupi marekebisho katika masoko ya fedha yanaweza kuwa machungu. Watu wana wasiwasi juu ya fedha zao walizowekeza na pia wafanya kazi wa makampuni husika. Kwa muda mrefu ujao nina imani masoko yetu ya fedha yanaweza kujibadilisha na ni yenye uthabiti, yanaweza kukabiliana na mabadiliko hayo."
Huko Marekani, masoko yalikuwa yakingojea leo kama kampuni kubwa la bima,AIG, hatima yake itakuwa kama ile ya benki ya uwekezaji ya Lehman Brothers iliofilisika. Wasiwasi unaendelea katika masoko ya fedha na hisa. Benki kuu ya Marekani, na zile za Ulaya, Uengereza na Japan kwa pamoja zilitia dola bilioni 210 katika masoko ya fedha hii leo ili kuyapiga jeki masoko yenye kutoa mikopo.
Masoko ya hisa mjini London na Tokyo yalipoteza kwa asilimia nne hii leo, kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa zaidi ya miaka mitatu, na soko la Wall Street huko New York jana lilipata hasara ya zaidi ya asili mia nne.
Macho yote yanakodolewa sasa kwa Benki Kuu ya Marekani kuona kama itaweza kuupunguza mbinyo pale utakapotangazwa uamuzi baadae leo juu ya vima vya riba kwa mikopo. Kuna tetesi kwamba kima cha riba kwa mikopo kitapunguzwa kwa hadi asilimia 0.075 . Tetesi hizo zimepata ukali baada ya bei ya mafuta kupungua, hivyo kupunguza wasiwasi wa kutokea mfumoko wa bei za bidhaa. Leo pipa moja la mafuta liliuzwa dola 90, kukihofiwa kwamba hali ya uchumi kwenda chini kutapunguza mahitaji ya mafuta. Thamani ya Dola ya Kimarekani ilipungua leo thamani yake ukilinganisha na Yen ya Japan.
Waziri wa fedha wa Marekani, Henry Paulson, aliapa jana kwamba atahakikisha kunakuweko utulivu na nidhamu katika masoko ya fedha huko nchini mwake na pia katika nchi za ngambo. Hata hivyo, alitahadharisha:
"Tutauvuka mzozo huu sio kwa siku moja na sio bila ya mshtuko mkubwa."
Naye Dominique Strauss-Kahn, mkuu wa Shirika la Fedha Duniani, IMF, amesema mzozo huu wa fedha duniani haujesha na mabenki zaidi yanaweza kufungwa, hivyo kutoweka mabenki huru ya uwekezaji. Alisema ule ukweli kwamba mabenki yanajirekebisha kusipelekee kuweko hamkani. Hata hivyo, alisema mambo haya yanapelekea wasiwasi na mivutano katika masoko ya fedha na ni jambo ambalo linaweza likatokea. Alisema dunia inakabiliana na mzozo wa kifedha usiowahi kuonekana, kwa vile unatokea kwenye moyo wa mfumo wa fedha, yaani Marekani, na sio katika nchi za pembeni, na umeiathiri dunia yote kwa wakati mmoja.