1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa jaribio la mauaji dhidi ya Trump atiwa mbaroni

Sylvia Mwehozi
16 Septemba 2024

Vyombo vya habari nchini Marekani vimemtaja mshukiwa katika kile ambacho shirika la upelelezi FBI limesema lilikuwa jaribio la kutaka kumuua mgombea wa urais wa chama cha Republican Donald Trump siku ya jumapili.

Maafisa usalama katika uwanja wa Gofu wa Trump
Maafisa usalama katika uwanja wa Gofu wa TrumpPicha: CHANDAN KHANNA/AFP via Getty Images

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, Ryan Wesley Routh ametajwa kuwa mshukiwa aliyejaribu kumuua Trump, tukio ambalo lilitokea jana Jumapili.

Ryan aliwahi kufanyiwa mahojiano na shirika la habari la AFP mwaka 2022 huko mjini Kyiv Ukraine, ambako alisafiri kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za vita. Ripoti za vyombo vya habari zinasema mshukiwa huyo ndiye aliyekamatwa baada ya maafisa wa idara ya ulinzi wa viongozi ya Secret Service kufyatua risasi dhidi ya mtu aliyekuwa amebeba bunduki la Ak-47 karibu na uwanja wa gofu wa mjini Florida ambako Trump alikuwa akicheza.

Mshukiwa huyo alikuwa ametoka kwenye kichaka alichokuwa amejificha na kutoroka kwa gari jeusi kabla ya kufuatiliwa na mamlaka.

Polisi akionyesha bunduki ya Ak-47 aliyokutwa nayo mshukiwa wa jaribio la mauaji dhidi ya TrumpPicha: Joe Raedle/Getty Images/AFP

Vituo vya utangazaji vya CNN na CBS vimeripoti kwamba Ryan ni fundi ujenzi wa nyumba za bei nafuu aliyejiajiri huko Hawaii ambaye ana rekodi ya kukamatwa kwa miongo kadhaa na kutoa machapisho ya mara kwa mara kuhusu siasa na matukio ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kumkosoa Trump, mgombea urais wa Republican. Wakati mmoja, mshukiwa huyo anadaiwa kuwa aliwahi kuelezea uungaji mkono wa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi ulioanzishwa na rais Vladimir Putin wa Urusi.

Soma: FBI yasema Trump alilengwa katika jaribio la mauaji

Shirika la habari AFP lilimhoji Ryan mjini Kyiv mwishoni mwa Aprili mwaka 2022, alipokuwa akishiriki katika maandamano ya kuwaunga mkono wananchi wa Ukraine waliokwama katika mji wa bandari wa Mariupol.  Aliieleza AFP wakati huo kwamba "Putin ni gaidi, na anahitaji kukomeshwa, kwa hivyo tunahitaji kila mtu kutoka ulimwenguni kote kuacha kile wanachokifanya na kuja hapa sasa".

Baada ya kufanikiwa kumdhibiti mshukiwa huyo, idara ya Secret Service ilisema hapo jana kwamba Trump yupo salamakama alivyoeleza mwakilishi wake Rafael Barros.

"Rais wa zamani Donald Trump yuko salama na hajadhurika kufuatia tukio lililotokea mchana wa siku ya Jumapili kwenye Klabu ya Gofu ya Kimataifa ya Trump huko West Palm Beach. Wafanyakazi wa idara ya Secret Service walimfyatulia risasi mtu aliyekuwa na bunduki karibu na uwanja na suala hili liko chini ya uchunguzi."

Donald Trump huko Las VegasPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Katika ujumbe wake kupitia mitandao ya kijamii, Trump alitoa shukrani kwa kila mtu, polisi na idara ya Secret Service kwa kumlinda dhidi ya tukio hilo ambalo ni la pili na limetokea chini ya miezi miwili. Katika jaribio la kwanza mgombea huyo alipigwa risasi alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni huko Pennsylvania, na kujeruhiwa sikio lake la kulia.Donald Trump yuko salama baada ya "jaribio la kuuawa."

Matukio yote mawili yanaangazia changamoto za ulinzi wa wagombea urais katika kipindi hiki cha kampeni zenye ushindani mkali huku zikiwa zimesalia takribani wiki saba kabla ya uchaguzi wa Novemba 5.

Rais Joe Biden amekemea kitendo hicho akisema siasa za Marekani hazina nafasi ya machafuko na kuiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kutumia kila rasilimali kumlinda Trump.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW