Msikiti wa Hagia Sophia wafunguliwa rasmi Istanbul
24 Julai 2020Adhana ilisikika mapema Ijumaa ikiwaita waumini wa dini ya kiislamu kuswali, wakati mamia ya waumini walipojikusanya nje ya msikiti huo ambao ulikuwa kanisa katika karne ya sita.
Kutokana na ufunguzi wa msikiti huo, barabara nyingi za kufika katika eneo hilo zilifungwa huku polisi 21,000 wakitawanywa kuimarisha usalama. Gavana wa Istanbul Ali Yerlikaya aliwaomba watu kufika kwenye nyumba hiyo ya ibada wakiwa na vitu vitatu pekee, Barakoa, misala ya kuswalia, uvumilivu na uelewa.
Katika mkusanyiko huo kwenye msikiti, hatua za kuweka umbali kati ya mtu na mtu ili kujikinga na virusi vya corona zilipuuzwa. Watu walikalia taulo na misala kati ya msikiti huo wa Hagia Hagia Sophia na msikiti wa Bluu ambao ni eneo jingine la kihistoria.
Erdogan ahudhuria ibada ya mchana
Rais Recep Tayyip Erdogan, ambaye atahudhuria ibada ya mchana huu, alitembelea msikiti huo jana alhamisi akiongozana na mkewe Emine kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho. Hapo, alama ya kijani iliyonakshiwa kwa maandishi ya dhahabu kwa lugha ya kituruki, kiarabu na kiingereza ilifunuliwa ikisomeka: Msikiti mkuu wa Hagia Sophia.
Historia ya msikiti huo ilianzia mwaka wa 537 ulipojengwa kama kanisa na kuwa kanisa kubwa zaidi la kikristo duniani. Hadhi yake ilibadilishwa mnamo mwaka 1934 kwa amri iliyotiwa sahihi na muasisi wa Jamhuri ya Uturuki Mustafa Kemal Ataturk, Hata hivyo, Julai 10, Baraza la taifa,na mahakama ya juu ya Uturuki iliibatilisha amri hiyo iliyosainiwa na Atartuk.
Saa kadhaa baadaye, Erdogan alitia sahihi amri ya kulifanya jengo hilo kuwa nyumba ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu, akisema kuwa ndoto yake ya ujanani imetimia.
Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO Umoja wa Ulaya na viongozi wengine wa makanisa wameelezea wasiwasi wao kuhusu mabadiliko ya hadhi ya msikiti huo huku Rais Erdogan akisisitiza kuwa Hagia Sophia ni haki ya kihistoria ya Uturuki.
Pamoja na hayo, Erdogan aliahidi kuuacha wazi msikiti huo kwa ajili ya watalii na kuwakaribisha watu wa Imani nyingine ambapo tofauti na awali hakutakuwa tena na kiingilio cha kuuona Msikiti huo.