1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimu wa 50 Bundesliga waaza rasmi

25 Agosti 2012

Marco Reus alipachika bao wakati akiichezea kwa mara ya kwanza mabingwa Borussia Dortmund katika Bundesliga, wakati msimu wa 50 wa ligi hiyo ulipofunguliwa rasmi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Werder Bremen.

Logo 50 Jahre-Bundesliga
Bundesliga yatimiza miaka 50

Reus aliuelekeza mkwaju wake katika kona ya lango la Bremen katika dakika ya 11 na kukipa kikosi cha kocha Juergen Klopp mwanzo mzuri katika ligi wakati wakilenga kupata taji la tatu mfululizo la Bundesliga.

Mchezo wa jana usiku ulikuwa wa kihistoria , kwani ni timu hizo mbili ndio zilizokuwa uwanjani miaka 50 iliyopita wakati Bundesliga ikizaliwa, tarehe 24 August mwaka 1963. Na pia Borussia Dortmund ikawa timu ya kwanza kupachika bao la kwanza katika Bundesliga. Jana haikuwa tofauti kwani historia imejirudia baada ya Borussia Dortmund kuwa wa kwanza kutikisa nyavu katika msimu huu wa jubilee, miaka 50 ya Bundesliga.

Marco Reuss wa Borussia DortmundPicha: Reuters

Walitoka jasho kupata ushindi

Lakini katika mchezo wa jana , mabingwa Dortmund ilibidi kupigana kiume wakati wote wakiendeshwa mbio na Bremen na wanaweza kujihesabu kuwa na bahati kuweza kutoka uwanjani na points zote tatu.

Ulikuwa mchezo mkali tangu mwanzo hadi mwisho, lakini ni faraja kuweza kushinda mchezo kama huo, amesema kocha wa mabingwa hao watetezi , Jurgen Klopp. Sijawahi kuona kikosi cha Bremen ambacho kimetulia kama hiki. Wameonyesha kuwa wanauwezo wa kusakata kandanda, na wanaweza kuleta madhara. Ameongeza kocha huyo wa mabingwa Dortmund.

Wachezaji wa Werder Bremen wakimzonga Marco Reuss wa DortmundPicha: Getty Images

Ameongeza Klopp kuwa , na hapa namnukuu, Tumo katika awamu ambamo hatujaweza kuwa na uhakika na baadhi ya mbinu uwanjani na tunafahamu kuwa tuna mengi ya kufanya, mwisho wa kumnukuu.

Kocha wa Bremen Thomas Schaaf, amesema kuwa , tumethibitisha kuwa sisi ni wageni wazuri kwasababu tumeacha points tatu hapa na hili linakera. Tulicheza vizuri lakini tumefanya makosa kidogo na ndio sababu tunaondoka hapa bila point.

Ligi yatimua vumbi tena

Ligi inaendelea leo jioni wakati Bayern Munich itakapoanza kazi ya kuwania kuuondoa ubingwa kwa Borussia Dortmund baada ya kuukosa kwa misimu miwili mfululizo, wakikaribishwa na Greuther Fuerth iliyopanda daraja msimu huu. Borussia Moenchengladbach inawakaribisha Hoffenheim , FC Augusburg ina miadi na Fortuna Dusseldorf ambayo nayo imerejea tena katika daraja la kwanza baada ya muda mrefu kufurukuta katika daraja la pili. Hamburg SV ina kwaana na Nuremberg wakati Freiburg itaonyeshana kazi na Mainz. Pia Wageni wengine kutoka daraja la pili Eintracht Frankfurt wanawakaribisha Bayer Leverkusen, wakati VLF Wolfsburg wanasubiriwa na VFB Stuttgart mjini Stuttgart. Jumapili itakuwa zamu ya Schalke 04 wakikaribishwa nyumbani na Hannover 96.

Nayo Premier League

Na huko katika ligi ya Uingereza Manchester United itaumana na Fulham leo jioni, wakati Tottenham Hotspurs wana kibarua na West Bromwich Albion. Chelsea ina miadi na New Castle, wakati Arsenal inakwenda Stoke City kesho Jumapili.

Mwandishi: Sekione Kitojo /dpae/rtre

Mhariri: Amina Abubakar

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW