Msimu wa 50 wa Bundesliga kuanza
20 Agosti 2012Timo Konietzka alifunga bao la kwanza la ligi hiyo mpya lakini hakuna ushahidi wowote wa picha za gazeti wala televisheni za kuonyesha bao hilo lililofungwa katika dakika ya kwanza.
Lakini kinyume chake, mchuano wa Ijumaa hii, utarushwa moja kwa moja kwenye televisheni za hapa nchini, pamoja na kompyuta, vifaa kama vile simu. Ligi ya Bundesliga imekuwa ni taasisi ya kitaifa ikiwa na rekodi ya wastani ulimwenguni ya uhudhuriaji wa mashabiki tangu ilipoanza kwa mwendo wa pole, kuponea sakata za kupanga mechi katika mika ya sabini na kuwatengeneza mashujaa kama vile Franz Beckenbauer, Gerd Mueller, Wolfgang Overath na Guenther Netzer.
Msimu wa kwanza wa Ligi ulikuwa na timu 16 kabla ya ligi kukua hadi tmu 18 na kwa kipindi kifupi timu 20 katika miaka ya mapema ya tisini ili kuzijumuisha timu za Mashariki ya Ujerumani baada ya muungano wa nchi hiyo. Bayern ambayo ilijiunga na ligi hiyo katika mwaka wa 1965, ndiyo iliyoshinda mataji 21 ikilinganishwa na matano kila mmoja ya mahasimu wake wa karibu Borussia Dortmund na Borussia Moenchengladbach.
Idadi ya mashabiki wanaohudhuria mechi uwanjani imepanda kutoka kiwango cha chini kabisa cha 17,468 katika mwaka wa 1972-73 hadi kiwango cha juu cha rekodi 45,116 katika kila mechi ya msimu uliopita, ikiwa ni rekodi ya ulaya ambapo mashabiki milioni 13.8 kwa jumla wakihudhuria mechi katika viwanja vya kisasa.
Vilabu vinapata mamilioni ya euro kutoka kwa tiketi lakini hata zaidi kutoka kwenye biashara ya mauzo ya bidhaa za vilabu na haki za televisheni. Mishahara ya wachezaji imefikia viwango vipya baada ya watu kama vile Seeler kupata dola 788 tu katika nyakati za mwanzo, na uhamisho unaotarajwia wa euro milioni 40 wa kiungo wa Uhispania Javier Martinez kutoka Athletic Bilbao na kujiunga na Bayern Munich unakuja miaka 36 baada ya Cologne kuwa klabu ya kwanza kutumia kitita cha tarakimu saba kumpata Mbelgiji Roger van Gool
Klabu ya Ujerumani ya Borussia Moenchengladbach inalenga kurejea katika jukwaakubwa kabisa la soka ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 34 wakati itakapopambana na Dynamo Kiev katika mechi za mchujo za kufuzu katika ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kivumbi hicho cha kesho chenye mikondo miwili pamoja na Agosti tarehe 29 kinaanza na mechi ya nyumbani kwa timu hiyo ya Ujerumani ambayo mara ya mwisho kucheza katika dimba hilo ilikuwa katika msimu wa mwaka wa 1977-78, na kubanduliwa nje ya nusu fainali dhidi ya Liverpool ambao pia waliibwaga katika fainali ya mwaka wa 1977.
Mechi kumi za mchujo zimepangwa kwa jumla kukamilisha awamu hiyo ya 32 ambayo droo yake itafanywa Agosti 30. timu hizo ni pamoja na Spartak Moscow v Fenerbahce, Braga v Udinese na Malaga v Panathinaikos.
Uingereza haijawakilishwa mara hii kwa sababu Chelsea walifuzu moja kwa moja kama mabingwa washikilizi wa kombe hilo, na kisha aliyemaliza wa nne katika ligi kuu ya Uingereza akaepuka mechi za mchujo. Moenchengladbach ilishinda mataji matano ya Bundesliga, kombe moja la shirikisho na vikombe viwili vya UEFA wakati wa enzi zake za miaka ya sabini. Ilimaliza katika nafasi ya kushangaza ya nne katika msimu uliokamilika wa Bundesliga na wanataraji kupata nafasi katika awamu ya makundi ijapokuwa waliwapoteza wachezaji wake Marco Reus na Dante ambao walijiunga na Borussia Dortmund na Bayern Munich.
Mwandishi: Bruce Amani/dpa
Mhariri: Othman Miraji