1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msuguano wazidi kati ya pande mbili za uongozi wa Taliban

16 Septemba 2021

Msuguano katika uongozi wa Taliban umeongezeka tangu kundi hilo lilipounda baraza la mawaziri lenye misimamo mikali wiki iliyopita linaloambatana zaidi na uongozi wao wa sheria kali wa miaka ya tisini.

Taliban-Sprecher Sabiullah Mudschahid
Picha: Xinhua /imago images

Mvutano huo umetokea faraghani lakini uvumi ukaanza kuenea kwa haraka kuhusu makabiliano ya vurugu ya hivi karibuni kati ya pande hizo mbili za kundi la Taliban katika kasri ya raisi unaojumusiha madai kwamba kiongozi wa pande yenye misimamo ya wastani Abdul Ghani Baradar ameuawa. Uvumi huo ulifikia kiwango ambapo kanda ya sauti na taarifa iliyoandikwa kwa mkono inayodaiwa kutoka kwa Baradar mwenyewe, ikikana kwamba alikuwa ameuawa. Siku ya Jumatano, Baradar alionekana kwenye mahojiano katika televisheni ya taifa akisema  kwamba alikuwa safarini kutoka Kabul kwa hivyo hakuwa na uwezo wa kufikia vyombo vya habarikukanusha habari hizo. Alilihakikishia kundi ka Mujahedeen, wazee na vijana kutokuwa na hofu na kwamba hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.

Msemaji wa kundi hilo la Taliban Zabihullah Mujahid amekanusha kuweko kwa mgawanyiko wowote katika uongozi huo. Siku ya Jumanne, waziri wa mambo ya nje wa uongozi huo wa Taliban Amir Khan Mutaqi, alikanusha ripoti hizo na kuziita uvumi.

Amir Khan Muttaqi - Waziri wa mambo ya nje wa uongozi wa TalibanPicha: Bilal Guler/Anadolu Agency/picture alliance

Wakati huo huo, katika taarifa aliyochapisha kupitia mtandao wa twitter Alhamisi (16.09.2021) msemaji mmoja wa kundi hilo la Taliban Suhail Shaheen amesema kuwa mkutano kati ya Deborah Lyons, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan na waziri wa mambo ya ndani Sirajuddin Haqqani uliangazia zaidi kuhusu msaada wa kibinadamu.

Shaheen amesema kuwa Haqqani alisisitiza kuwa maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaweza kuendelea na shughuli zao bila vikwazo vyovyote na kutoa msaada muhimu kwa Waafghanistan.

Macron kukutana na Merkel

Haya yanatokea wakati rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, akitarajiwa kumkaribisha  kansela wa Ujeumani Angela Merkel Alhamisi  jioni kwa mkutano wa kikazi katika makao rasmi ya rais huyo katika kasri ya Elysee mjini Paris.

Kwa mujibu wa duru ya kasri hiyo, mkutano huo utakaondaliwa wakati wa dhifa ya chakula cha jioni, utaangazia hali ilivyo nchini Afghanistan na katika eneo la Sahel. Pia watazungumzia kuhusu urais wa Ufaransa unaotarajiwa wa baraza la Umoja wa Ulaya. Ufaransa inachukuwa urais huo wa kupokezana wa miezi sita mnamo mwezi Januari.

Huku hayo yakijiri, China, Alhamisi  inatarajiwa kuandaa mkutano wa viongozi wa Kusini na Kati mwa Asia kwa njia ya video kuzungumzia kuhusu hali nchini Afghanistan. hata hivyo haikubainishwa wazi iwapo Afghanistan ambayo ni mwanachama mwangalizi wa shirika la ushirikiano la Shanghai itakuwa na waakilishi kutoka kwa uongozi wa Taliban.