Msumbiji yautangaza upya utalii wake
14 Oktoba 2022Rais wa Msumbiji Philipe Nyusi amefungua rasmi Maonyesho ya kimataifa ya utali mjini Maputo yanayokusudiwa kufufua tena sekta hiyo ya utalii ilioshuka kwa asilimia 98 kutokana na mashambulizi ya makundi ya kigaidi pamoja na janga la Uviko 19 liloipiga taifa hilo kwa miaka miwili iliopita.
Akifungua maonyesho haya ya kimataifa ya utalii rais wa Msumbiji Phillipe Nyusi amesema Kauli mbiu ya maonyesho haya ni Utalii kama kigezo cha Kuinua Uchumi na ni biashara ya kifahari na kituo cha mikutano kati ya mashirika ya utalii ya kitaifa na taasisi za wenzao kufika hata Australia na sehemu nyengine za ulimwengu.
"Baadhi ya sehemu za Cabo Delgado zimepoteza utalii kutokana na ugaidi unao tokea huko lakini sasa tunataka kuwarejesha watalii sehemu hiyo sababu ni sehemu iliokua na vivutio vingi vya utalii." alisema.
Rais Nyusi amesema majeshi ya nchi rafiki yalioko eneo la Cabo Delgado sasa yameanza kuwarejesha raia wa Msumbiji katika sehemu zao walizozihama.
Soma Zaidi:Wakuu wa SADC walaani uasi nchini Msumbiji
Nae waziri wa utalii na utamaduni wa Msumbiji Aldevina Materula anasema 98% ya utalii wa Msumbiji umeharibika kutokana na vita vya magaidi na tatizo la Uviko19 katika kipindi cha miaka miwili iliopita .
"Kwa kweli uliharibika sana, hasa tulikua tukikabiliwa na vita viitatu kwa wakati mmoja ukitaja magaidi Kaskazini na pia mkoa wa kati na pia Uviko 19. Na Capo Delgado iko juu juu zaidi katika pembe ya Kaskazini mwa Msumbiji."
Waziri Materula anasema masafa yaliopo kutoka Maputo mkoa wa Kati waliopo hadi kufika Capo Delgado ni sawa na masafa kutoka Lisbon Ureno hadi Helsinki nchini Iceland kwahivo watu wakilifahamu hilo wataweza kuja Msumbiji kutembelea maeneo mengine mazuri yakuvutia .
Amesema tayari wameshasaini mikataba kadha na mataifa ya jirani kuweza kukuza utalii katika eneo la mataifa ya nchi za kusini mwa Afrika. "Hivi karibuni tulisaini mkataba na Afrika Kusini pamoja na taifa la Eswatini kukuza utalii katika nchi zetu tatu na tena tunaweza kuwasiliana kwa Lugha moja. Tunaamini itakua muhimu sana sana sio tu kwa Msumbiji lakini eneo lote la kusini mwa Afrika."
Moja ya tatizo linaloikumba Msumbiji sasa ni deni kubwa serikali ilionalo kuliendesha shirika la ndege la Msumbiji LAM na bado majadiliano yanaendelea kuona iwapo shirika hilo la ndege litabinafshwa kwa wawekezaji
Maonyesha ya kukuza utalii wa Msumbiji yataendelea hadi siku ya Jumamosi ijayo.
OMAR MUTASA DW MAPUTO